Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ummy asimamisha wanne Shinyanga

Ca0653ecb15e9d0d916b0884fc06dcb0.jpeg Ummy asimamisha wanne Shinyanga

Sun, 30 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Ummy Mwalimu amewasimamisha kazi kwa wiki mbili watumishi wanne wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kupisha uchunguzi wa kuwepo kwa ubadhirifu katika ujenzi wa machinjio ya kisasa katika halmashauri hiyo.

Watumishi waliosimamishwa juzi baada ya kutembelea na kukagua mradi wa machinjio ni Mchumi Gwakisa Mwakyeba, Mkuu wa Idara ya Mifugo, Tito Kagize, Mhandisi wa Ujenzi, Kasimu Thadei pamoja na Mkuu wa Idara ya Manunuzi, Godfrey Mwangairo.

Baada ya kupewa taarifa na Mkurugenzi wa Hamashauri ya Shinyanga, Geofrey Mwangulumbi, Ummy alisema taarifa za mradi huo anazo kutoka kwa Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) kuwa kuna ubadhirifu wa fedha kwenye machinjio hayo. Alishangaa watu waliohusika kutochukuliwa hatua.

“Mkurugenzi wewe ni mteule wa Rais hivyo sitakugusa kwenye suala hili saizi yangu ni hawa watumishi hivyo kuanzia sasa na wasimamisha kazi wiki mbili ili kupisha uchunguzi juu ya ubadhirifu wa ujenzi wa machinjio hii ya kisasa,” alisema Ummy.

Aliagiza watumishi wengine ambao wameshahamishwa, wapelekwe katika halmashauri hiyo kujibu ubadhirifu wa ujenzi wa machinjio hii ya mifugo ya kisasa pamoja na wakandarasi wachukuliwe hatua.

Waziri Ummy alisema gharama za ujenzi wa machinjio hiyo anazifahamu ni Sh bilioni 5.7 na zimeshatumika Sh bilioni 5.1 . Alitaka kufahamu zilipo Sh milioni 600 wakati mradi ukiwa haujakamilika na kutakiwa kuongezwa Sh. millioni 172 kutoka kwenye mapato ya ndani.

Akitoa taarifa ya ujenzi wa machinjio, Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Mwangulumbi alisema gharama za mradi huo awali ilikuwa ni Sh. bilioni 5.9, lakini zilipungua hadi Sh. bilioni 5.5 huku akibainisha kuwa Sh milioni 600 zipo.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk Philemon Sengati alisema suala la watumishi hao atalifanyia kazi na watatoa taarifa juu ya watumishi hao ndani ya wiki mbili.

Chanzo: www.habarileo.co.tz