Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Umepata kulisikia kabila la Wandorobo?

E69d6f900b176e906e12bca52da8ad05 Umepata kulisikia kabila la Wandorobo?

Sun, 28 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WANDOROBO ni kabila dogo sana miongoni mwa makabila yanayoishi katika Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, katika maeneo ya Ngapapa, Leruk na Napilukunya.

Pia wanapatikana wilayani Simanjiro katika vijiji vya Kitwai A, Kitwai B, Komolo, Loiborsoit B, Loborsiret na Lormorjoi. Hata hivyo, Wandorobo ni wachache sana na wanahesabika.

Kwa viwango vya dunia ya sasa Wandorobo ni maskini sana kwani hawana tabia ya kuweka akiba ya chakula wala mifugo, hawajengi wala kulima, hawatilii maanani suala la elimu wala kujishughulisha na masuala ya serikali kwa namna yoyote.

Pia jamii ya Wandorobo imeshindwa kuongezeka kutokana na mila zao na desturi potofu ambazo pia zinachangiwa na hali mbaya ya uchumi wa kabila hili.

Baadhi ya mila na desturi hizo ni kwa mwanamke wa jamii ya Wandorobo anapopata ujauzito, hujitokeza mwanamume wa jamii ya Wamasai na kujitolea kulea mimba hiyo kwa kutoa ng’ombe, ili endapo atazaliwa mtoto wa kike basi atalazimika kuolewa na mfugaji huyo.

Kutokana na utaratibu huo wa wanawake wa jamii ya Wandorobo kuozwa kwa makabila ya kifugaji ili kupata mifugo, imekuwa vigumu kwa vijana wa kabila la Wandorobo kupata mwanamke wa kuoa, na hivyo idadi yao kuzidi kupungua.

Asili yao

Yapo machapisho ambayo yanabainisha kuwa jamii ya Wandorobo ndio wakazi wa asili wa Mkoa wa Tanga. Pengine kutokana na tabia yao ya kuhamahama imewafanya wajikute wakiwa wakazi katika maeneo ya Manyara, na pengine Arusha na Singida.

Hata hivyo, jamii hii haitaki kuitwa Wandorobo, wanataka waitwe ‘Akiye’, kwa sababu wanaamini kuwa jina la Ndorobo ni la kupachikwa tu. Zipo dhana mbili; moja inasemwa kuwa jina hili walipewa na majirani zao Wamasai, likimaanisha “watu wasiokuwa na kitu”.

Lakini pia ipo dhana ya kuwa jina hili la Wandorobo lilitokana na tabia yao katika ulaji wakati wa uwindaji wao, kwani ni hodari sana kwa kutumia mishale. Mshale mmoja wa Mndorobo kuua wanyama wawili kwa mpigo si jambo la ajabu.

Mara nyingi, wanapowinda huwalenga zaidi wanyama wanaonyonyesha. Mara wanapomwona mnyama wa aina hiyo humpiga mshale na anapoanguka hukimbilia kunyonya maziwa yake na damu yake kama afanyavyo mdudu ndorobo anaponyonya damu ya binadamu au mifugo.

Ndorobo ni mdudu (nzi pori mkubwa) anayeng’ata mifugo hususan ng’ombe na kuambukiza magonjwa ya malale au nagana.

Mndorobo pia akimpiga mshale mnyama huanza kwa kunyonya maziwa na akitosheka hutafuta mshipa unaotoa damu na kuinyonya damu hadi ashibe. Baada ya hapo ndipo huchukua kibuyu chake wanachokiita ‘ululu’ na kukijaza.

Baadaye Mndorobo hurudi nyumbani ambako humchukua mkewe na wanawe na kurudi kwenye windo lao ambalo hulichuna na kulila huku wakitunza ngozi, mafuta na mifupa kwa matumizi ya baadaye.

Makazi na utamaduni wao

Kwa kiasi fulani Wandorobo ni watu wanaopenda kuishi porini. Huishi kwa kutegemea kurina asali na wanapenda kuvaa kiutamaduni; kipande cha ngozi ya nyama (lusira) au kaniki, ikiwa imefunikwa sehemu tu ya mwili wake.

Hata hivyo, kwa sasa jamii ya Wandorobo imebadilika na huvaa nguo kulingana na mavazi yanayovaliwa na jamii ya Wamasai. Wandorobo kwa sasa hawajui lugha yao isipokuwa wanazungumza Kimasai, kutokana na kuzungukwa na kabila hilo kwa eneo kubwa, na pia kutokana na kulitegemea kabila hilo katika maisha yao.

Nywele za Wandorobo huwa ndefu na hupendelea kuzivuta kwa nyuma. Kwa wanaume mara zote utamwona Mndorobo akiwa ameshika upinde, podo la mishale ubavuni na kishoka ambacho wenyewe hukiita ‘kitodyo’ mkononi.

Kwa kawaida Wandorobo ni watu wa kuhamahama, mara msitu huu mara ule na chakula chao kikuu ni nyama za porini, mizizi na asali.

Kunapotokea ukame jamii ya Wandorobo hulazimika kuponda mizizi wanayoiita ‘kisherembwa’. Huitumia mizizi hiyo kama maji kutokana na kwamba mizizi hiyo kuwa na maji mengi.

Pia wakati wa ukame hutumia mizizi hiyo kama chakula kwani matunda aina ya ‘ndungu’ waliyozoea kula kama chakula chao hukauka huko porini.

Aidha, yapo matunda mengine ya porini yatokanayo na mimea kama ‘ngabaito’ na ‘olugumu’ ambayo pia hutumika kama chakula. Na wakati wa mvua Wandorobo hujisitiri kwa kujenga mabanda ya ngozi za wanyama, mfano wa mahema.

Jamii ya Wandorobo haina tofauti na jamii ya Wahazabe (Watindiga) wanaoishi katika eneo la Yaenda Chini katika Wilaya ya Mbulu, kwani maisha yao ni ya kuhamahama kutoka eneo moja hadi eneo jingine ili kutafuta chakula na maji.

Tiba ya maradhi

Jamii ya Wandorobo haina desturi ya kuhudhuria katika zahanati, kituo cha afya au hospitali kwa ajili ya kupata matibabu ya maradhi. Na hata wajawazito wanaotaka kujifungua hutumia dawa za asili zitokanazo na miti mbalimbali kwa ajili ya kujitibu.

Katika kukabiliana na maradhi mbalimbali kulingana na mazingira wanayoishi, jamii ya Wandorobo imekuwa ikitumia dawa mbalimbali kama mti wa ‘mukutani’, dawa ambayo wanatumia kwa ajili ya maradhi ya minyoo, tumbo na kuondoa nyongo mwilini.

Inasemwa kuwa mti wa mukutani hupondwa na kisha kunywa maji yake na humfanya aliyekunywa atapike nyongo, pamoja na kuua minyoo tumboni.

Pia mafuta ya mti wa ‘ndemwee’ hutumika kwa kuchanganya na asali, na kuwa dawa ya kutibu maradhi ya kifua. Mti wa ‘singwai’ hutumika kutibu maradhi ya tumbo na kuzuia kuharisha, na mti wa ‘osiamali’ hutumika kama dawa ya kutibu maradhi ya tumbo.

Dawa nyingine za miti shamba zinazotumiwa na jamii ya Wandorobo ni mti wa ‘sogonoi’ ambao huutumia kama dawa ya malaria, homa na tumbo. Na mizizi ya jamii ya Olduvai hutumika kama dawa ya magonjwa ya zinaa.

Pamoja na dawa hizo za kunywa, kuna dawa nyingine za kujipaka ili kuepuka madhara ya wanyama wakali. Dawa kama ‘mberesero’ na ‘ormudee’ ambazo zinasemekana husahaulisha ama kupoteza eneo ambalo mtu anataka kufika, na pia zinaweza kumsafirisha bure katika vyombo vya usafiri.

Inasemwa kwamba unaweza kuzitumia dawa hizo kwa kuchoma moto na kisha kuzungushia majivu yake mahali ulipo, ama kuzitwanga na kuweka mdomoni ili kila unayezungumza naye akubaliane na wewe kwa jambo lolote.

Inadaiwa kuwa dawa hizo hutumiwa na majangili wakati wanapokwenda kuwinda wanyama kwenye misitu ya hifadhi, ambako hujizungushia dawa hizo ili wasiweze kuonekana na askari wa hifadhi hizo, huku majangili hao wakiwaona askari hao wa hifadhi.

Tabia ya ujasiri

Kwa asili Wandorobo ni mashujaa wa aina yake, si waoga kabisa, na hivyo hawapendi au kujali sana umoja. Mtu na mkewe wanaweza kukaa porini kwa miaka bila hofu wala kuhitaji msaada wa watu wengine.

Inaaminika pia kuwa wana uwezo mkubwa wa kutumia miti shamba kuyatawala mazingira yao kiasi cha wanyama wakubwa kama simba, chui na majoka kuwakimbia.

Kuna simulizi nyingi za miujiza ya watu wa jamii ya Wandorobo. Moja ni ile inayosimulia juu ya wawindaji saba walioingia katika msitu mmoja mkubwa kwa matarajio ya kupata wanyama.

Si kwamba hawakufanikiwa tu, bali pia walipotea mchana kutwa wasiweze kujua njia ya kurudi kwao. Ulipofika usiku, wakiwa wamekata tamaa waliona mbuyu mkubwa wenye pango kwenye shina, ambalo lingetosha kuifadhi watu kumi na wa tano au zaidi.

Wawindaji hao waliingia katika pango hilo kwa matarajio ya kuupitisha usiku. Ikatokea kuwa pango hilo lilikuwa makazi ya joka kubwa aina ya chatu.

Baadaye joka lilirejea na kuingia pangoni humo na hivyo wawindaji wale, kwa hofu kubwa walitimka mbio kila mmoja akijaribu kuokoa roho yake.

Kumbe muda wote ule, katika eneo hilo, alikuwepo Mndorobo mmoja aliyekuwa akiwatazama. Mndorobo huyo aliwaita na kuwataka watulie kisha akaenda kwenye pango lile la mbuyu na kutamka maneno kadhaa.

Mara kwa mshangao wa wawindaji wale joka lile lilitoka taratibu na kutokomea porini. Mdorobo akawataka wawindaji kurejea pangoni na kulala bila wasiwasi wowote. Walilala na kesho yake wakafanikiwa kupata njia ya kurudi kwao.

Ili kuburudika na kufurahia maisha, jamii ya Wandorobo hujiburudisha kwa kutengeneza pombe ya kienyeji inayotengenezwa kwa asali. Pombe hiyo huitwa ‘huumi’ na hutumika zaidi katika sherehe mbalimbali wanazozifanya katika maeneo yao.

Makala haya yametokana na vyanzo mbalimbali vya habari.

0685 666964 au [email protected]

Chanzo: habarileo.co.tz