Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Umeme wakwamisha uzinduzi mradi wa maji Ngara

Fri, 17 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ngara. Tatizo la kukatika mara kwa mara kwa umeme kumekatiza hafla ya uzinduzi wa mradi wa maji katika Shule ya Sekondari Baramba wilayani Ngara mkoani Kagera kutokana mashine za kusukuma maji kushindwa kufanya kazi.

Uongozi wa Shirika la Marafiki wa Afrika (MAT), uliotekeleza mradi huo kwa gharama ya zaidi ya Sh130 milioni umelazimika kusitisha kwa muda hafla ya uzinduzi uliopaswa kuongozwa na mbunge wa jimbo la Ngara, Alex Gashaza kusubiri kurejea kwa huduma ya nishati ya umeme.

Akizungumza shuleni hapo leo Agosti 17, 2018 wakati wa hafla ya kuadhimisha miaka 20 ya shirika hilo linalojishughulisha na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya jamii wilayani Ngara, Padri Isias Bambara amesema uzinduzi huo utafanyika mara umeme utakaporejea na mtambo kuweza kusukuma maji.

“Tunakuomba mheshimiwa mbunge urejee ukumbini kuendelea na shughuli nyingine za maadhimisho ya jubilee ya miaka 20 ya shirika hadi umeme utakaporejea ndipo ukamilishe uzinduzi wa mradi wa maji,” amesema Padre Bambara ambaye ni Mwenyekiti wa MAT

Amesema kuhairisha kwa muda uzinduzi hadi umeme utakaporejea kunalenga kuuthibitishia umma wa shule na wananchi wa maeneo jirani kuwa mradi huo unatoa maji.

Kwa mara ya kwanza, Shirika la MAT lilianza nchini mwanzoni mwa mwaka 1981 likiwa chini ya Wamisionari wa Kanisa Kotoliki kutoka Ujerumani wakishirikiana na wenzao wa jimbo la Rulenge wakati huo ikiongozwa na marehemu Askofu Christopher Mwoleka kwa lengo la kueneza Injili kupitia jumuia ndogo ndogo jimboni humo.

Mwaka 1998, MAT ilianza kutekeleza miradi ya maendeleo ya jamii katika sekta za afya, maji, elimu na shughuli za ujasiriamali wilayani Ngara ili kuboresha huduma kwa jamii ikishirikiana na mashirika na taasisi za Twaweza, Tacaids, NELSAP na Tasaf chini ya ufadhili wa Shirika la Marafiki wa Afrika Ujerumani, Red Charity na Serikali.

Chanzo: mwananchi.co.tz