Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Umado wataka maelekezo ya jiji yaheshimiwe

0a7ae26edb64ce8cec2fd0fa652edf50.png Umado wataka maelekezo ya jiji yaheshimiwe

Mon, 1 Mar 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

UMOJA wa Masoko Rasmi Jijini Dodoma (Umado), umewataka wafanyabiashara wa matunda, mbogamboga na viazi kutoka nje ya Mkoa wa Dodoma, kuheshimu na kutekeleza maelekezo yanayotolewa na Halmashauri ya Jiji kwa mujibu wa sheria ikiwemo ya kushusha mizigo kwenye soko la kisasa la Ndugai.

Ushauri huo umetolewa na viongozi wa umoja huo jijini hapa wakati wakiwafafanulia waandishi wa habari kuhusu katazo lililotolewa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma linalowataka wafanyabishara wanaopeleka mizigo yao huko kwa kutumia magari, kushusha mizigo yao katika Soko la Ndugai.

Makamu Mwenyekiti wa Umadu, Goha Magwai, alisema kinachotakiwa wafanyabiashara wote wakiwamo kutoka nje ya Dodoma hawana budi kutii maelekezo yaliyotolewa na halmashauri hiyo ili wafanye kazi kwa ufanisi.

“… Hakuna sababu ya kuvutana na halmashauri kuhusu katazo hilo, kinachotakiwa ni kutoa mapendekezo kuhusu namna inayoweza kuboresha utendaji,” alisema.

Kwa mujibu wa Magwai, serikali imewekeza fedha nyingi katika Soko la Ndugai kwa ajili ya wafanyabishara wadogo na wakubwa, wanapaswa kushirikiana kutatua changamoto zinazojitokeza.

Mwenyekiti wa Umado, Marwa Mabucha, aliiomba halmashauri kuboresha eneo wanalotakiwa kushushia mizigo ikiwa ni pamoja na wafanyabishara wanaoleta biashara kutoka nje ya mkoa, kupewa sehemu ya kuuzia bidhaa zao, badala ya kulazimika kuzisafirisha hadi katika masoko mengine.

“Tunaiomba halmashauri ya jiji, ituboreshea eneo hili tunaloshushia mizigo ili tuweze pia kuuza biashara baada ya kushusha mizigo, badala ya kupeleka yote kwenye masoko mengine,” alisema.

Mfanyabiashara katika soko la matunda na mbogamboga la Bonanza, Fortunatus, alishauri halmashauri kukaa na wafanyabishara kujadili na kutatua changamoto zinazojitokeza.

Ofisa Masoko wa Jiji la Dodoma, Jemes Yuna, alisema kwa nyakati tofauti katika mazungumzo na wafanyabiashara wanaoleta biashara hizo kwa kutumia magari, kuwa wanawajibika kufuata maelekezo kama inavyostahili.

“Badala ya kuvutana kati yao na halmashauri badala yake watumie vikao vinavyoweza kuleta majibu yatakayowafanya kufurahia soko hilo tofauti na hali ilivyo sasa,” alisema.

Alisema hakuna mgogoro na wafanyabishara kutoka nje ya mkoa, ingawa baadhi yao wamekuwa wakikaidi maelekezo ya halmashauri.

Chanzo: habarileo.co.tz