Matukio ya ukatili yakiwamo mauaji yamekuwa yakiitesa Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, chanzo cha hayo kikitajwa kuwa ulevi na uvutaji bangi.
Wilaya hii iliyo mpakani mwa Tanzania na Kenya inakabiliwa na matukio ya ukatili ambayo ni kinyume cha haki za binadamu.
Ingawa hakuna takwimu sahihi za matukio hayo, kati ya Juni na Septemba mwaka huu, yametokea makubwa manne ambayo gazeti hili limeandika taarifa zake.
Matukio makubwa
Kijana mfanyakazi wa ndani, alidaiwa kumuua mwajiri wake Rogasian Onesfory (60), mkazi wa Kijiji cha Ubetu wilayani hapa Juni 25, mwaka huu.
Ilielezwa Onesfory alitoka kwenda kuuza nguruwe akapata Sh800,000.
Baada ya kijana wa kazi kujua hilo, anadaiwa alimuua kwa kumkata kwa panga kichwani. Mwili wake alikwenda kuutupa kwenye shimo la choo na kutoroka na fedha hizo.
Julai 7, mwaka huu, Melania Tarimo (32) na mume wake walikamatwa na polisi wakidaiwa kuhusika na mauaji ya mtoto.
Wanadaiwa kumchinja mtoto wao wa miezi minne, kuzika kichwa na kuficha kiwiliwili katikati ya magodoro kwenye chumba walichokuwa wakiishi.
Tukio hilo lilitokea katika Kijiji cha Nayeme wilayani Rombo likihusishwa na wivu wa mapenzi na ulevi.
Agosti 29, mwaka huu mkazi wa Kijiji cha Ngaseni wilayani hapa, Anord Tarimo (30), aliuawa kwa kukatwa kwa panga na kijana aishiye Kijiji cha Kwalakamu aliyemfuata ofisini kwake kuomba msaada wa chakula.
Mwanamume huyo, fundi nguo eneo la soko jipya la Usseri aliuawa muda mchache baada ya kumnunulia chakula kijana huyo aliyedai alikuwa na njaa kutokana na hali ngumu ya maisha.
Kijana Deogratius Shirima (26), mkazi wa Kijiji cha Lessoroma wilayani Rombo, katika tukio lingine anadaiwa kumuua mama yake mzazi, Doris Shirima (51) kwa kumkata kwa panga shingoni akijaribu kuokoa nyumba anayoishi isibomolewe na kijana huyo.
Hilo lilitokea Septemba mosi mwaka huu, na kuzua simanzi kwa wananchi kijijini hapo na maeneo ya jirani.
Kauli ya mkuu wa wilaya
Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Kanali Hamis Maiga, alisema amelazimika kuwakutanisha viongozi mbalimbali, wakiwamo wa vijiji na kata kuangalia namna ya kukabiliana na matukio hayo.
Pia, anasema kwa kushirikiana na viongozi wa dini watakaa kuweka mikakati ya pamoja ya kuyadhibiti.
"Tuliita kikao tukakutana na wenyeviti wa vitongoji, vijiji, kata na tarafa. Tumezungumzia masuala haya yanayoendelea ya ukatili kwenye jamii na mambo mengine.
"Kwa hiyo, tumekaa nao ili waweze kukutana na viongozi wote wa dini katika wilaya hii tukomeshe ukatili unaotokea kwenye jamii zetu," alisema.
Emma Moshi, mtendaji wa Kijiji cha Lessoroma alisema matukio mengi yanayotokea wilayani hapa yanatokana na vijana kujiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya ikiwamo bangi.
"Huku kijijini matukio yamekuwa ni mengi, vijana hawana kazi za kufanya wanavuta bangi bila woga, hili limekuwa kero," alisema.
Maoni ya wadau
Wakizungumzia chanzo cha matukio ya mauaji, wadau wa maendeleo na wale wa haki za binadamu wanasema mengi yanasababishwa na ukosefu wa ajira unaochangia vijana wajiingize katika makundi mabaya yakiwamo ya uvutaji bangi na ulevi.
Virginia Silayo, mkurugenzi wa shirika lisilokuwa la kiserikali linalojihusisha na haki za binadamu la Ajiso, alisema ni wakati sasa kwa Serikali kuiangalia kwa jicho la pekee Wilaya ya Rombo kutokana na matukio ya ajabu ambayo yamekuwa hayaishi kwenye jamii.
Alisema matukio mengi yanayotokea yanasababishwa na ulevi wa pombe na uvutaji bangi ambao udhibiti wake ni mdogo.
"Wanaofanya mauaji katika Wilaya ya Rombo wengine si akili zao za kawaida, unakuta kijana anamkata shingo mama yake bila woga. Hili linatokana na hali iliyopo kwenye jamii, vijana wamejisahau baada ya kujiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya na mambo mengine.
"Ni lazima tufanye utafiti lakini pia jamii ijitambue. Mwenyekiti wa kijiji na mtendaji wajue ni nini kinaendelea au kuna watu gani ambao hawaeleweki. Ni lazima tukae chini tuliangalie hili," alisema.
Anashauri Serikali kuangalia ni kwa namna gani vijana watawezeshwa ili kujipatia kipato kwa kutumia fursa zinazowazunguka.
“Wawezeshwe kufanya kazi kwa kutumia rasilimali zinazopatikana katika mazingira yao. Kufanya hivyo kutawaongezea kipato, hivyo kuwaondoa katika makundi ya ulevi na uvutaji wa bangi,” anasema.
Viongozi wa dini
Sheikh wa Wilaya ya Rombo, Eliamini Mvungi anasema viongozi wa dini wanaendelea kutoa elimu kwa jamii misikitini na hata makanisani.
Hata hivyo, anasema changamoto iliyopo ni kukengeuka kwa jamii ambayo imemwacha Mungu.
"Kwenye jamii kumekuwa na watu ambao hawaeleweki, suala la ulevi wa pombe na bangi limekithiri wilayani hapa; haya yanachangia kwa kiasi kikubwa matukio ya ukatili kwenye jamii zetu," alisema Sheikh Mvungi.
"Tunaendelea kuelimisha jamii hasa watu wamjue Mungu, maana kutomjua Mungu ni chanzo pia cha watu kufanyiana ubaya katika jamii. Tukiwa kwenye mihadhara mara kwa mara tunatoa elimu kwa jamii na hata walimu kule mashuleni tunawaomba watusaidie na tumekuwa tukitoa elimu huko ili angalau jamii iweze kubadilika."
Mchungaji wa Kanisa la Global Congregation for Christ Tanzania, Aban Moshi alisema chanzo cha matukio ya ukatili kwenye jamii ni vijana kukosa ajira na kujiingiza katika matukio yasiyofaa ikiwamo uvutaji bangi na ulevi.
"Kuna tabia ambazo watu hujifunza kutokana na makundi rika, kuna kundi ambalo wanafanya hivyo na hata wale wanaokuwa wanaiga na kufanya vivyo hivyo.
“Pia, watu kukosa kazi ya kufanya, kukata tamaa na wakati mwingine wazazi kutowajibika ipasavyo kwa watoto huchangia matukio ya ajabuajabu kuendelea kutokea kwenye jamii," alisema.