Ucheshi na ukarimu anaposikiliza kero na mahitaji watu wanaoingia ofisini kwake kumuona, ni sifa ya kipekee inayombeba Ofisa elimu maalumu wa Wilaya ya Kilolo, Biliel Maketa.
Mwenyewe anasema ulemavu wake wa macho haukumzuia kutimiza ndoto zake.
“Tangu nikiwa mdogo nilijua kama sitajibidiisha kupata kile ninachohitaji sitoweza kutimiza ndoto zangu,” anasema.
Haikuwa kazi ngumu kukutana naye hasa nilipoomba nafasi hiyo kutokana na kazi zake hasa kampeni ya kusaka watoto wenye ulemavu waliofichwa, kusikika nje na ndani ya wilaya hiyo.
Ubunifu huo sio tu kwamba umempa heshima, bali umewafanya baadhi watoto waliokuwa wamenyimwa haki yao ya msingi ya kupata elimu, kuingia darasani.
Wakati alipoanza darasa la kwanza katika shule ya Msingi Makalala iliyopo Mafinga wilayani Kilolo, hakujua kama siku moja atakuwa ofisa elimu.
Anasema hali ya maisha ya familia yao ilimpatia nguvu ya kukazana kusoma, pamoja na kukutana na mazingira magumu katika kujifunza
“Kusema kweli nilikuwa sioni na ilikuwa kazi kubwa kujifunza. Nilitamani kuacha shule, lakini nilipowaangalia wazazi wangu nilijiona kabisa kwamba, natakiwa nitimize ndoto zangu ili nije kuwasaidia,” anasema mwalimu Maketa.
Anasema ilimlazimu kutumia mbinu ya kusomewa katika mchakato wake wa kujifunza akiwa darasani.
Alimpata mwanafunzi mmoja mwaminifu na mwenye uwezo darasani, akawa anamsaidia kumsomea. Kazi kubwa kwake ilikuwa kukariri kile anachosomewa.
“Kwa hiyo nimefanikiwa kusoma kwa kusomewa na wenzangu. Mwalimu akishaandika ubaoni rafiki zangu wananisaidia kusoma au nikihitaji kusoma mwenyewe pia, nasaidiwa,” anasema.
Mwalimu Maketa anakabiliwa na ulemavu wa macho kwa uoni hafifu.
Mtaalamu na mwalimu wa watoto wenye ulemavu wa macho wilayani Kilolo, Katindasa Justine anasema uoni hafifu una athari kitaaluma ikiwa mtoto mwanafunzi hatosaidiwa.
“Ulemavu wa macho unahitaji msaada wa karibu, kama mwanafunzi haoni basi walau unapofundisha uongee kwa sauti ya juu ili mwanafunzi asikie, huenda hiyo ikawa nafuu yake kwenye elimu,” anasema.
Maketa anasema alikuwa akijitahidi kuhudhiria vipindi vyote na kusikiliza kile mwalimu anachofundisha, ili hata anaposomewa na wenzake iwe rahisi kuelewa.
Anasema haikuwa rahisi kwake kupelekwa shule za watoto wasioona kulingana na mazingira yaliyokuwapo kwa wakati huo. “Nilimaliza darasa la saba nikafaulu vizuri; huo ulikuwa mwanzo wa mafanikio yangu,” anasema.
Anasema alijiunga na masomo ya sekondari katika shule ya Mpwapwa ambako aliendelea na mtindo huohuo wa kusomewa.
“Hapa nilikuwa na mtu mmoja tu wa kunisomea. Ilikuwa changamoto, lakini nia yangu ilikuwa moja tu, kutimiza ndoto zangu,” anasema na kuongeza:
“Siku zote nilijitahidi zaidi kusikiliza walimu wanachofundisha hiyo ilinisaidia kufanya vizuri darasani.”
Anasema alimaliza kidato cha nne na kuamua kusomea ualimu.
“Changamoto za uoni zilinifanya nisomee elimu maalum, kwa sababu najua mahitaji ya watoto wenye ulemavu ni makubwa na anayeweza kuwasaidia ni yule anayewafahamu zaidi,” anaeleza.
Maketa alijiunga na Chuo cha Ualimu cha Patandi alipohitimu masomo ya cheti na stashahada kabla ya kuanza kufundisha.
Anasema baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Sebastian Kolowa na kuhitimu shahada ya kwanza ya ualimu akibobea katika fani ya elimu maalumu.
Anasema alianza kazi akifundisha shule mbalimbali, ikiwamo ya walemavu iliyokuwa Ilula wilayani Kilolo.
Anasema siku moja akiwa kwenye harakati zake za kufundisha, alipigiwa simu akitakiwa kuripoti kwa ofisa elimu wa Wilaya ya Kilolo.
“Nilipokuja kuripoti nikashangaa kuambiwa nimechaguliwa kuwa ofisa elimu maalum wa wilaya hii. Ni jambo la kumshukuru Mungu,” anasema.
Anasema kiuhalisia hakuna mafanikio bila bidii hata kama njia za kufikia mafanikio hayo zina miiba.
Hata hivyo anasema uhaba wa miundombinu rafiki kwa ajili ya watoto wenye ulemavu, ni changamoto aliyokuwa anakabiliana nayo.
Anasema ingekuwa rahisi kwake kujifunza kupitia karatasi zenye maandishi maalum kwa watu wenye ulemavu wa macho, lakini kwa wakati huo haikuwezekana.
Mwalimu Maketa anasema mkakati wake mkubwa wilayani Kilolo, ni kusimamia elimu na kuhakikisha hakuna mtoto mwenye ulemavu anayekosa masomo.
Anasema ni rahisi kutekeleza malengo hayo akishirikiana na wenzake, wakiwamo viongozi, walimu na wadau wa elimu.
“Mfano kwa sasa napambana kuona tunapata mabweni na madarasa ya kutosha na yenye miundombinu stahiki kwa watoto wenye ulemavu,” anasema.
Kampeni ya kuwasaka watoto walemavu
Ofisa elimu huyo anasema kupitia sensa ya kuwasaka watoto waliofichwa ili waanze masomo, amegundua bado jamii inahitaji elimu kuhusu watu wenye ulemavu.
“Niliweza kutimiza ndoto kwa sababu wazazi wangu walinipa msaada, hivyo hata nilipokwama, walitafuta njia za kunisaidia. Wazazi wanayo nafasi kubwa kuhakikisha watoto wao wenye ulemavu wanatimiza ndoto zao,” anaeleza.
Anasema ulemavu sio ugonjwa kwamba hatoweza kumudu masomo kwa sababu ya ulemavu wake.
“Tukiachilia mbali ulemavu wa akili, ambao pia unaweza kumfundisha mtoto elimu ya kujitegemea, kila mtoto anaweza kutimiza ndoto zake kama atawezeshwa,” anasema.
Anasema mara kadhaa amekuwa akikutana na wazazi wenye watoto walemavu ili kuwatia moyo, kwamba wakiwekeza kwenye elimu watoto hao hawatakuwa mzigo kama wanavyodhani.
Anasema kama mtoto hatosaidiwa kufikia malengo yake, anaweza kuwa mzigo kwa sababu hata atakapokuwa mtu mzima bado ataendelea kuwa tegemezi.
“Kwa hiyo natamani kuona Kilolo yenye watoto walemavu wanaopata haki yao ya msingi kabisa ya kupata elimu,” anasimulia.
Ofisa elimu huyo anasema ukombozi kwa kundi la watu wenye ulemavu utakuwapo ikiwa kila mtoto anayestahili kuanza masomo yake atapata nafasi ya kusoma.
“Ndio maana mkakati pekee wa wilaya ya Kilolo ni kuhakikisha watoto wote walemavu wanaanza shule, kwa sababu tukiwaacha ni mzigo kwa wazazi wenyewe, wilaya na hata Taifa,” anasema.