Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ukweli katili katika ajali lori la mafuta iliyotokea Msamvu

71458 Lori+pic

Thu, 15 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Takriban watu 71 wameripotiwa kufariki dunia, wengine 70 ni majeruhi katika ajali ya lori la mafuta eneo la Msamvu, Morogoro. Mungu azilaze pema peponi roho za marehemu, awaponye majeruhi ili warejee mitaani kuijenga nchi yao.

Nini chanzo cha ajali? Ni lori la mafuta kuanguka. Watanzania walipoona limeanguka waliona ni fursa ya kimaisha. Wakavamia na kuanza kuchota mafuta. Hapa ndipo pa kujadili na kuusema ukweli katili unaoumiza. Waingereza huita ‘the brutal truth’.

Anayeusema ukweli katili ni mkweli katili. Nachagua kuwa hivyo (the brutal honesty). Baada ya hapo tuliseme tatizo bila kuzunguka mbuyu, kwamba chanzo cha madhara haya ni hali za Watanzania.

Kuna mambo makuu matano ambayo yanakupasa kuyabeba katika mjadala. Anza na hili, gari limepata ajali, Watanzania wawili, dereva na utingo wanalia msaada. Watanzania makumi wanafika kwenye gari na kuanza mikakati ya kuchota mafuta. Hawawasaidii wanaoomba msaada. Huu ni ukosefu wa utu.

Gari lilikuwa linasafirisha mafuta. Mali ya mtu. Watanzania wanaona gari lenye mafuta ya Mtanzania mwenzao, hawatoi msaada wa ulinzi, wanaanza kupora. Hapo kuna matatizo mawili; wizi na ukosefu wa utu.

Watanzania gani waliopoteza maisha na kujeruhiwa? Jibu lake linakupa jambo la tatu. Maskini ndio waliopata madhara. Ni sawa kusema kuwa familia za kimaskini ndizo zilizopokea madhara makubwa kwa ndugu zao kufariki dunia na kujeruhiwa.

Habari zinazohusiana na hii

Gari limepata ajali na limebeba petroli, watu wanalivamia bila tahadhari na kuanza kuichota. Hili ni tatizo la ufahamu kuhusu hatari ya magari ya mafuta, ingawa limeandikwa ni “hatari”.

Gari hata la kawaida, linapopata ajali huwa na uwezekano mkubwa wa kushika moto, ndio maana hushauriwa kuwahi kuchomoa betri. Sasa gari ni la mafuta. Tatizo hapa ni elimu ya madhara ya magari ya mafuta.

Ajali imetokea mjini Morogoro. Eneo ambalo ni rahisi mno kwa vyombo vya usalama kufika na kutoa msaada. Ukipima muda ambao gari lilipata ajali na madhara makubwa yaliyotokea, utaona kuwa vyombo vya usalama, jeshi la zimamoto na polisi, walichelewa kufika eneo la tukio, ama kwa kuchelewa kupata taarifa au kupuuza.

Iweje polisi na zimamoto wachelewe kupata taarifa? Hawafanyi doria? Waliona lakini wakadharau kwa kudhani lori lisingelipuka? Namba zao za simu za wito wa dharura hazifahamiki kwa watu? Au watu wanajua namba lakini hawakuona kuwa ni tatizo la kupiga namba za dharura kuomba msaada?

Majibu ya maswali hayo kwa namna yoyote ile, yatatuleta kwenye neno moja; uzembe!

Na neno hilo uzembe lina matawi yake, kwamba polisi na zimamoto ni wazembe kuchelewa kufika eneo la tukio kutoa msaada. Ni wazembe kwa kutofikisha inavyotakiwa elimu ya majanga ya ajali za moto kwa wananchi.

Je, ajali hiyo ya lori la mafuta ndio ya kwanza nchini? Hapana. Tanzania imeshapitia ajali kadhaa za namna hiyo. Tatizo ni moja kuwa watu husahau na vyombo vya ulinzi na usalama vikiona hali imetulia navyo vinastarehe. Hata hii ya Msamvu, Morogoro litapita, watu watastarehe. Elimu ya kukabiliana na majanga, haijawahi kuwa muhimu nchini.

Baada ya ajali kutokea Morogoro, ‘majaji na mahakimu’ wa mitandaoni, walithubutu kutamka kuwa waliofariki dunia walijitakia. Kwamba waliona lori la mafuta wakaenda kwa tamaa zao.

Kuna ambao walikuwa pembeni, waliwamo mama lishe, janga likawafuata. Hawa nao wanasemwa walijitakia.

Dhahiri, watoa maoni hayo mitandaoni walionesha kukosa utu kulikovuka mpaka. Watanzania wamefikia hatua ya kuwasimanga waliopata majanga.

Madhara ya ajali ya lori la mafuta Morogoro yanaainishwa ndani ya mambo matano, ambayo ni ukosefu wa utu, wizi, umaskini wa Watanzania, kukosekana kwa elimu ya majanga na uzembe.

Suala jingine ni umaskini. Shida zina kawaida ya kujenga usugu. Ndio maana waliokufa na kujeruhiwa ni maskini. Wapo waliofahamu madhara lakini walijaribu bahati yao. Walijitoa mhanga.

Chanzo: mwananchi.co.tz