Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ukuta Mirerani wasaidia Serikali kukusanya Sh1.43bilioni

57021 Pic+mirerani

Tue, 14 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Serikali imekusanya Sh1.43 bilioni za madini ya Tanzanite kuanzia Aprili hadi Desemba mwaka huu baada ya kujengwa ukuta katika machimbo ya madini  hayo Mirerani.

Mtendaji mkuu wa tume ya madini, Profesa Shukrani Manya amesema hayo leo Jumapili Mei 12 na kueleza kuwa makusanyo hayo ni mara saba ya yale ya awali.

Ukuta huo uliojengwa kuzunguka eneo lenye ukubwa wa kilometa 24.5 ujenzi wake uligharimu Sh6 bilioni  lengo likiwa ni kuzuia wizi wa madini na ukwepaji kodi.

Akizungumza katika mafunzo ya waandishi wa habari kuhusu sekta ya madini, Profesa Manya amesema mapato hayo yamekusanywa kutoka kilogramu 781.2 za madini hayo.

Amesema mwaka 2016 walikusanya kilo 164.6 zilizozalisha Sh71.8 milioni wakati mwaka 2017 wakikusanya kilo 164.6 zenye thamani ya Sh166.1 milioni.

"Kwa hiyo ujenzi wa ukuta umesaidia kuongeza mapato na kudhibiti madini yaliyokuwa yakipotea, haya ni mafanikio na mwaka huu 2019 tunatarajia kuongeza mapato zaidi," amesema  Profesa  Manya.

Pia Soma

Amesema tathmini yao kwa mwaka huu katika kila wiki kilo kati ya 20 mpaka 25 hupitishwa getini jambo lililosababisha kuongeze zaidi wathaminishaji.

"Tumepeleka wathaminishaji zaidi kutoka Dodoma," amesema Profesa Manya.

Amesema kwa sababu marekebisho ya sheria ya madini yanataka kuwepo kwa masoko ya madini tayari masoko hayo yamefunguliwa kwenye mikoa 20.

"Tangu Machi 27 mwaka huu tulipofungua soko la Geita tayari kilo 167 za madini zimepitishwa sokoni," amesema.

Profesa Manya amesema masoko hayo yatasaidia kupata takwimu sahihi za madini nchini na kwamba changamoto wanayokabiliana nayo kwa sasa ni uhaba wa watumishi.

Awali, mkurugenzi wa sheria,  Edwin Igenge amesema mabadiliko ya sheria ya madini ya mwaka 2017 yamesaidia kuongeza udhibiti wa madini.

Amesema mabadiliko hayo yanamlazimisha mchimbaji kushirikiana na Watanzania katika kazi zake na kama kuna utaalamu zaidi utamuhitaji mtu kutoka nje ya nchi lazima waseme kwa muda gani Watanzania watapata utaalamu huo na kuchukua nafasi.

Chanzo: mwananchi.co.tz