Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ukioga, kufua kwenye chanzo cha maji faini Sh1 milioni

39483 Pic+kuoga Ukioga, kufua kwenye chanzo cha maji faini Sh1 milioni

Mon, 4 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Mtu yeyote atakayekutwa na kosa la kuosha, kufua, kuoga na kusababisha au kuruhusu kitu kuingia kwenye miundombinu ya maji atakabiliwa na faini ya Sh50,000 au isiyozidi Sh1 milioni ama kifungo cha mwezi mmoja gerezani.

Adhabu hiyo imeainishwa katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Huduma ya Maji na Usafi wa Mazingira wa mwaka 2018 uliowasilishwa jana bungeni na Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa.

Hata hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imepinga adhabu hizo ikisema ni kubwa sana ikilinganishwa na uzito wa kosa ambalo lingehitaji tu kuelimishwa huku Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ikitaka kutenganishwa kwa adhabu.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mohamed Mgimwa alishauri kuwa sehemu ya makosa na adhabu ifanyiwe maboresho makubwa katika maeneo mbalimbali.

“(Pia) kutenganisha makosa yanayofanywa na mtu na yale yanayofanywa na taasisi kama vile kampuni za kibiashara pamoja na adhabu zake,” alisema.

Alisema kamati inaona ni vyema faini za makosa yanayomhusu mtu yapunguzwe huku yale yanayohusu taasisi faini yake iwe kati Sh5 milioni hadi Sh50 milioni.

Mgimwa alisema kwenye makosa yanayohusiana na mabomba ni vyema kuyatenganisha adhabu zake kulingana na ukubwa wa bomba linalohusika.

Pia, alisema ni vyema kutenganisha makosa na adhabu zake kulingana na matumizi ya maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na yale ya biashara.

Awali, akiwasilisha muswada huo, Profesa Mbarawa alisema unapendekeza uundwaji wa mamlaka za maji na usafi wa mazingira, muundo wake na hadhi yake kisheria pamoja na kazi na majukumu yake.

Akichangia muswada huo, mbunge wa Busega (CCM), Dk Raphael Chegeni alisema kilio cha wananchi ni kupata maji na kwamba matumizi ya maji katika Ziwa Victoria yako chini ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki.

Alisema tatizo analoliona ni utoaji wa fedha serikalini ambalo limesababisha miradi mingi ya maji iliyoanzishwa kutokamilika kwa wakati.

Mbunge wa viti maalumu (CCM), Hadija Aboud aliomba kuongeza vyanzo vipya vya mapato katika mfuko wa maji ili uweze kutatua changamoto ya maji mijini na vijijini.

Wakati huohuo, Serikali imeridhia mapendekezo ya Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria ya kufuta sehemu ya tatu na nne ya Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali namba 4 wa mwaka 2018 ili iendelee kufanyia kazi mapendekezo ya maeneo hayo.

Sehemu hizo ni ya tatu inayohusika na masuala ya pasipoti kupitia mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Mafao ya Kustaafu katika utumishi wa kisiasa na sehemu ya nne ya Sheria ya Pasipoti na Hati za Kusafiria.

Akiwasilisha muswada huo bungeni jana, mwanasheria mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi alisema baada ya majadiliano ya kina kati ya Kamati ya Bunge ya Sheria na Katiba na Serikali wameridhia kuondoa sehemu hizo.

“Serikali imetafakari kwa kina ushauri wa kamati na hatimaye imeridhia kwamba kwa sasa mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Mafao ya Kustaafu katika utumishi wa kisiasa ambayo ni sehemu ya tatu ya muswada yaondolewe,” alisema.

Miswada hiyo ilipitishwa na Bunge jana jioni.



Chanzo: mwananchi.co.tz