Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ukarabati wa Kibaha sekondari wakamilika

Kibahas Ukarabati wa Kibaha sekondari wakamilika

Thu, 11 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

SERIKALI imekamilisha ukarabati wa Shule ya Sekondari Kibaha mkoani Pwani kwa gharama ya Sh bilioni 1.6.

Vilevile katika mwaka wa fedha 2020/21, serikali imetoa Sh milioni 80 kwa ajili ya ujenzi wa bweni katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibaha.

Kauli hiyo ilitolewa Bungeni jana na Naibu Waziri Tamisemi, Dk Festo Dugange wakati akijibu swali la Mbunge wa Kibaha Mjini, Silvester Koka (CCM).

Koka alisema miundombinu ya maji katika Shirika la Elimu Kibaha, ilijengwa miaka 50 iliyopita kwa mabomba ya asbestos yasiyo rafiki kwa afya za wanadamu, lakini pia ni machakavu sana.

Alihoji ni lini serikali itatatua changamoto hii ya maji katika shirika hilo na ni lini serikali itakarabati majengo ya Chuo Cha Maendeleo ya Jamii (FDC) katika shirika hilo.

Dk Dugange alisema serikali inatambua uwepo wa mabomba ya maji ya kipenyo cha milimita 200 yenye urefu wa kilomita nne na kipenyo cha milimita 150 yenye urefu wa kilomita mbili, yaliyojengwa kwa asbestos tangu kuanzishwa kwa shirika hilo.

Hata hivyo, serikali ilikwishabadilisha bomba la asbestos lenye urefu wa kilomita 0.75 la kipenyo cha milimita 200 na bomba lenye urefu wa kilomita moja na kipenyo cha milimita 150 kuwa ‘PVC’. Serikali itaendelea kubadilisha mabomba hayo kulingana na upatikanaji wa fedha.

Alisema serikali imefanya tathmini ya ukarabati wa miundombinu ya majengo ya Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) cha Shirika la Elimu Kibaha, ambapo Sh bilioni 1.48 zinahitajika ili kufanya matengenezo.

Alisema, Shirika la Elimu Kibaha lilifanya ukarabati mdogo wa madarasa na jengo la utawala kwa kutumia mapato ya ndani, ambao uligharimu Sh milioni 25.73.

Chanzo: habarileo.co.tz