Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ukarabati makazi ya wazee wahitaji Sh10 bilioni

Tue, 26 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Serikali inahitaji Sh10.2 bilioni kwa ajili ya ukarabati wa makazi ya wazee yaliyopo sehemu mbalimbali hapa nchini ili kuwafanya nao wafurahie maisha yao ya uzee na kuwaweka salama dhidi ya vitendo vya mauaji ya vikongwe.

Hayo yamesemwa leo Machi 25 jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk John Jingu wakati wa mkutano wa wadau kuhusu mkakati wa Taifa wa kuondoa mauaji ya wazee.

Amesema mpaka sasa yapo makazi 17 ya wazee hapa nchini lakini makazi hayo ni chakavu na yanahitaji ukarabati mkubwa wa miundombinu ili wazee waishi vizuri na kufurahia maisha yao ya uzeeni.

“Kwa tathmini tuliyoifanya, tumeamua kuyapunguza makazi haya yabaki manane tu. Kwa hiyo ukarabati wa makazi hayo unahitaji Sh10.2 bilioni kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya vyoo, mabwalo na nyumba za makazi ya wahudumu,” amesema Dk Jingu.

Dk Jingu amewataka wadau kujadili namna ya kupata kiasi hicho cha fedha ili kuboresha makazi ya wazee na kuwanusuru na mauaji ya vikongwe yanayofanyika katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Kuhusu mauaji ya wazee, Dk Jingu amesema mauaji hayo yamepungua kwa kiasi kikubwa kutoka mauaji ya wazee 565 mwaka 2014 mpaka kufikia mauaji ya wazee 59 kufikia Julai mwaka jana.

Amesema Serikali imefanya mambo mbalimbali kuwalinda wazee ikiwemo kuandaa sera ya wazee, mkakati wa Taifa wa kuondoa mauaji ya wazee na mpango wa kuboresha maisha ya wasiojiweza (Tasaf).

“Hili suala si la Serikali pekee, wadau tunatakiwa kushirikiana kulinda maisha ya wazee wetu. Tuungane, wadau wa maendeleo, mashirika ya kimataifa, viongozi wa dini, asasi za kiraia, vyombo vya habari,” amesema.

Kwa upande wake, Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Dk Naftali Ng’onde amesema wameamua kupunguza makazi ya wazee kwa sababu baadhi ya makazi hayo wanaishi wazee wachache licha ya kwamba gharama za huduma kama vile umeme na maji kuendelea kutolewa kama kawaida.

“Jumla ya wazee 471 wanaishi kwenye makazi haya na Serikali inatenga bajeti yao kila mwaka. Baadhi ya makazi hayo yana watu wachache, kwa mfano pale Songea wapo sita, Lindi wapo wanane. Kwa hiyo, hawa wachache tutawahamisha kwenye makazi mengi ambayo tutayaboresha,” amesema.

Mkutano huo wa wadau ulioandaliwa na taasisi ya kimataifa ya Helpage, imewashirikisha pia wakuu wa wilaya za Kishapu, Misungwi, Nzega na Chato ambao kwa pamoja wamesema mauaji ya wazee yamepungua kwenye wilaya zao.

Mkuu wa wilaya ya Chato, Mtemi Simeon amesema mauaji katika wilaya yake yamepungua kutokana na mikakati ya Serikali katika kutoa elimu kwa wananchi na kuchukua hatua za kisheria kwa wote wanaobainika kujihusisha na matukio hayo.



Chanzo: mwananchi.co.tz