Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ukame waua mifugo 556 Longido

Ukame Ukame waua mifugo 556 Longido

Sat, 26 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ukosefu wa chakula na maji kwa ajili ya mifugo imesababisha mifugo 556 kufa wilayani Longido mkoani Arusha.

Takwimu hizo zimetolewa jana Ijumaa, Februari 25,2022 na Mkuu wa Wilaya ya Longido, Nurdin Babu katika hafla ya kukabidhi chakula kilichotolewa na Shirika World Vision kupitia mradi wa Ketumbeine (AP), ambapo amewataka wananchi wasibweteke na misaada hiyo kwa kuwa hivi sasa mvua zinanyesha.

Babu amesema kwa takriban miezi sita wilaya hiyo imekabiliwa na ukame uliosababisha vifo vya ng'ombe, kondoo na mbuzi 556 hivyo akashukuru msaada wa tani 20 za unga wa mahindi na maharage tani 5.

Amesema kutokana na ukame wananchi wamepungukiwa na chakula huku uzalishaji nao umepungua wilayani humo kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Babu amesema kutokana na janga hilo wamejipanga kuhakikisha katika kipindi cha mvua wanahamasisha wananchi katika shughuli za kilimo na kuwaelimisha namna ya kuweka akiba ya chakula na Serikali kupitia idara ya kilimo imetenga bajeti ya mbegu ili kuwasaidia kulima mazao yaliyo bora.

"Niwaombe wananchi wa Wilaya ya Longido kutokubweteka kwani misaada hiyo ya chakula haitakuwepo siku zote wachukue fursa ya msimu huu wa mvua kuendelea kupanda mazao ambayo yatawasaidia baadaye,"alisema Babu.

Advertisement Awali akitoa taarifa katika hafla hiyo Mratibu wa mradi wa Worldvision wa Ketumbeine(AP)Peruth Daud amesema zaidi ya kaya 900 katika tarafa ya Ketumbeine iliyoko wilayani Longido mkoani Arusha zimepatiwa chakula na shirika la world vision ili kupunguza janga la njaa.

DaudĀ  amesema chakula hicho ni maharage na unga wa mahindi ambapo wamepatiwa kupitia kata zilizopo katika tarafa hiyo ikiwemo Ketumbeine, Elangatadapash, Noondoto, Gilailumbwa, Gilabomba na Ilerienito.

Amesema jumla ya tani 20 za mahindi na tani 5 za maharage vyenye thamani ya Sh41.4 milioni na kunufaisha kaya 1000 ndani ya vijiji 19 katika Tarafa hiyo.

"Kila kaya nufaika itapata kilogramu 20 za unga wa mahindi na kilogramuĀ  tano za maharage ambapo watoto 3214 pia watanufaika,"amesema Mratibu huyo.

Naye mmoja wa wananchi wa Tarafa ya Kitumbeine ambaye pia ni kiongozi wa mila, Peter Mollel amesema mabadiliko ya hali ya hewa yamewaathiri na baadhi ya wanaume wamekimbia familia zao.

Imeandikwa na Teddy Kilanga, Arusha

Chanzo: www.tanzaniaweb.live