Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ujumbe wa Zainab na Saumu kwa Magufuli

32151 Pic+zainabu TanzaniaWeb

Tue, 18 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wakati aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Stella Manyanya alipotembelea Shule ya Msingi ya Mtinko iliyopo mkoani Singida mwaka jana, si yeye wala si uongozi wa shule hiyo aliyekuwa anajua jinsi wanafunzi wenye mahitaji maalumu wangeweza kumkabili waziri huyo.

Baada ya kufanya mazungumzo na uongozi wa shule hiyo na kutembezwa katika mazingira yake, ilikuwa ni wakati kwa mbunge huyo wa Nyasa kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye sasa na Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, kuwaaga wanafunzi wa shule hiyo.

‘’Ni upi ujumbe aliotaka aufikishe kwa Rais John Magufuli?’’, aliwauliza wanafunzi.

Wakati wanafunzi wasio na ulemavu wakisema kwamba wao wangetamani tu salamu zao zifikishwe tu kwa Raisi Magufuli, hali haikuwa hivyo kwa Zainab Maulid na Saumu Mustafa, ambao ni wanafunzi wenye ulemavu wa kutosikia.

Wanafunzi hao majasiri, kila mmoja aliwasilisha kwa waziri mahitaji ya msingi ambayo walitaka yashughulikiwe, ili kuboresha ustawi wa walemavu wenzao waliopo majumbani na shuleni pia.

Mmoja wao alimueleza waziri kuwa wanapata shida katika kusoma kwani ukosefu wa vyumba vya madarasa, husababisha wanafunzi wa madarasa tofauti kuchanganywa katika chumba kimoja. Alitaka hili litatuliwe ili waweze kusoma vizuri.

Mwingine kati ya hawa wawili aliomba ujenzi wa mabweni, huku akisema kuwa kuna watoto wengi wasiosikia wako majumbani na hawawezi kuja shule kwa kuwa hakuna miundombinu ya kutosha kuwaisaidia kujifunza.

Ufasaha na umakini wao wa kuwasilisha masuala haya kwa waziri, ulimgusa kila mtu akiwamo waziri mwenyewe.

Mahitaji yote mawili yalichukuliwa na Serikali na kuanza kufanyiwa kazi kwa ushirikiano na kamati ya maendeleo ya shule. Vyumba vinne vya madarasa tayari vimekwisha jengwa na mabweni mawili yakiwemo ya wanasichana na wavulana yenye uwezo wa kuchukuwa wanafunzi zaidi ya 160.

Kuanza kutolewa elimu ya mahitaji maalumu

Shule ya Msingi ya Mtinko ilianzishwa mwaka 1981 na kuanza kutoa elimu kwa wanafunzi viziwi mwaka 2010.

Hata hivyo, wakati huo hakukuwa na mwalimu mtaalamu katika eneo hilo la elimu. Kutokana na hali hiyo, wanafunzi wasiosikia walikuwa wanachanganyishwa na wanafunzi wa kawaida na kufundishwa na walimu wale wale.

Mwalimu Bernard Muna aliletwa katika shule Julai 2012 kwa ajili ya kusimamia kitengo cha elimu ya mahitaji maalumu. Hata hivyo, naye hakuwa na utaalamu kwenye suala la elimu kwa wanafunzi wasiosikia.

“Ni kwa bahati nzuri tu,” anaeleza Mwalimu Muna, “katika mwaka huo huo nilibahatika kuhudhuria mafunzo ya mwaka mmoja na kurudi hapa rasmi kuanzisha kitengo cha elimu ya mahitaji maalumu mnamo mwaka 2013.”

Shule ya msingi ya Mtinko kwa sasa ina darasa la kwanza, tatu na la nne, huku la pili likikosekana.

Shule ina jumla ya wanafunzi wasiosikia 10 na walimu watatu. Lakini kuna changamoto bado katika namna jamii inavyolichukulia suala la elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu, huku baadhi ya wazazi wakiwaficha watoto wao wenye ulemavu.

Hata hivyo, hali hii imezidi kubadilika siku hadi siku kutokana na juhudi ambazo shule na kamati yake wamekuwa wakizichukuwa katika kuihamasisha jamii juu ya umuhimu wa kuwapeleka watoto wao wenye ulemavu shuleni.

Fikra yakinifu

Nchini Tanzania, kama ilivyo kwa nchi ningine duniani, serikali ndio mwajibikaji wa kwanza wa kuheshimu, kulinda na kutimiza haki za kielimu katika nchi. Shule, kamati, vyama vya wanafunzi/wazazi na wizara ya elimu ndiyo taasisi za msingi za serikali ambazo zinaweza kuwajibishwa katika kutimiza lengo hili.

Hata hivyo, ruzuku ambazo shule hupokea huamuliwa na wizara ya fedha, wahisani, taasisi za fedha za kimataifa na wakati mwengine wachangiaji binafsi. Kuwajengea wanafunzi, watoto na jamii kwa ujumla siyo tu husaidia kupigania utolewaji wa elimu bora bali pia husaidia kujenga uwezo wa fikra yakinifu kwa walengwa husika.

Hiki ndicho mashirika yasiyo ya kiserikali ya Medo pamoja na Action Aid Tanzania wamekuwa wakifanya na ambacho matokeo yake katika shule ya msingi Mtinko ni ya kupigiwa mfano.

“Kama elimu hii ya wanafunzi kujuwa haki zao isingewafika Saumu na Zainab,” anakiri Mwalimu Muna, “tusingekuwa na haya majengo hapa shuleni kwetu.”

Kuwafundisha watoto haki zao za msingi kumetajwa kuwa ni njia bora ya kuhakikisha haki hizi zinapatikana na kuheshimiwa na mamlaka husika na jamii kwa ujumla.

Saumu, Zainab wanena

Saumu, mwenye umri wa miaka 20, anaamini kwamba elimu kuhusu haki za msingi za mwanafunzi inasaidia kumlinda mwanafunzi pale anapoona haki hizo zipo hatarini kukiukwa.

“Hiki ndicho kilinileta hapa shuleni,” anasema Saumu aliye na ndoto ya kuwa mfanyabiashara mkubwa siku za baadaye “Pia nilitaka kujuwa kusoma na kuandika ili niweze kuziongelea haki kwa watu wengi zaidi katika kuhakikisha zinalindwa.”

Saumu na Zainab, wanatambulika kama mashujaa miongoni mwa walimu na wanafunzi katika shule yao. Kitu pekee kinachomsumbua Zainab anayetamani kuja kuwa mwalimu ni kuona kwa nini watoto kama yeye hawataki kwenda shule, licha ya ukweli kuwa shule kwa wanafunzi wasiosikia zipo.

“Wazazi wanapaswa kuwaruhusu watoto wao wajiunge na shule kwani hiyo ni hatua nzuri ya kuwawezesha kuzijua haki zao na kuzipigania,” anashauri Zainab.



Chanzo: mwananchi.co.tz