Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ujenzi soko la kisasa Kisutu kuanza mwezi ujao

10321 Soko+pic TZW

Sat, 30 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imesaini mkataba na kampuni ya ujenzi ya Mohammed kwa ajili ya ujenzi wa soko la kisasa Kisutu.

Soko hilo litakaloanza kujengwa mwezi ujao litakuwa na uwezo wa kuchukua wafanyabiashara 1,500 na litakuwa na huduma nyingine muhimu zikiwamo za benki, mabucha, machinjio na maegesho ya magari.

Akizungumza wakati wa utiaji saini mkataba huo jana, meya wa manispaa hiyo, Charles Kuyeko alisema Sh13.48 bilioni zimetolewa na Serikali Kuu kwa ajili ujenzi wa soko hilo litakalo kuwa na ghorofa nne.

“Ndani ya miezi 18 soko hilo litakuwa limekamilika na kuwafanya wafanyabiashara kufurahia mazingira mapya tofauti na ilivyokuwa awali hasa katika msimu wa mvua,” alisema Kuyeko.

Alisema, “Kutokana na kuanza kwa ujenzi, wafanyabiashara waliopo katika maeneo haya wapatao 633 watahamia eneo la Mkunguni na stendi ya zamani ya Kisutu ili kupisha ujenzi.”

Meya Kuyeko alisema tangu mwaka 1964 Soko la Kisutu lilikuwa si rafiki katika kufanya biashara na kutokana na hali hiyo, Serikali imeamua kuliboresha.

Mbali na hilo, alisema mikakati iliyo mbioni ni kuyafanya machinjio ya Vingunguti kuwa ya kisasa na kwamba Sh8 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo.

Aprili 5, mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema alinukuliwa akisema kabla ya wafanyabiashara kuhamia maeneo yaliyotengwa ya Mkunguni na stendi ya zamani ya Kisutu, manispaa itatumia Sh138 milioni kuyaboresha.

Uboreshaji huo alisema ni wa ujenzi wa machinjio, miundombinu na mabanda ya biashara.

“Nawaomba mkafanye kazi hii kwa weledi, mkaikamilishe kwa wakati na mzingatie viwango na thamani ya fedha,” alisema Mjema.

Mkurugenzi wa kampuni ya ujenzi ya Mohamed iliyopewa jukumu la ujenzi wa soko hilo, Taher Jafferji aliahidi kulijenga kwa viwango na kulikamilisha kwa wakati.

“Muda ni mchache lakini nitahakikisha tunajenga kitu chenye ubora ili mwaka 2020 mwanzoni tufanye sherehe za ufunguzi,” alisema.

Mmoja wa wafanyabiashara katika Soko la Kisutu, Mohammed Doula alisema kujengwa upya kutachangia kusogeza huduma karibu hivyo kuwawezesha kujiongezea kipato.

“Ni hatari kutembea na fedha mfukoni, lakini benki zikiwekwa katika eneo hili itakuwa ahueni. Kwa uwepo wa machinjio kwa wenzetu itakuwa rahisi kupata bidhaa,” alisema Doula.

Alisema hata wafanyabiashara wanaopanga bidhaa barabarani watapata nafasi ya kufanya shughuli zao ndani ya soko litakapokamilika.

Chanzo: mwananchi.co.tz