Mwanza. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe ametembelea na kukagua miradi minne ya ujenzi wa meli mpya, Chelezo na ukarabati wa Mv Victoria na Butiama katika Bandari ya Kusini jijini Mwanza na kueleza kuridhishwa na hatua zilizofikiwa.
Akiwa katika miradi hiyo leo Ijumaa Juni 22, 2019, Waziri Kamwelwe amesema tayari wakandarasi wa miradi hiyo wameshalipwa Sh58 bilioni kati ya Sh122.8 bilioni gharama ya mradi mzima.
“Nimeridhishwa na kasi waliyonayo wakandarasi hawa hususani ujenzi wa meli mpya, kuanzia Julai, 2019 makontena zaidi ya 300 yenye vyuma vya ujenzi wa meli hii yanaanza kupakiwa kutoka Korea kuja hapa nchini (Tanzania),” alisema Kamwelwe
Meli mpya ikikamilika itakuwa na uwezo wa kusafirisha abiria 1,200 na tani 400 ya mizigo kati ya Bandari ya Bukoba na Mwanza ambapo ujenzi wake umekamilika katia hatua za michoro, ukataji wa vyuma na kuagiza vifaa kutoka Korea.
Hafla ya kutia saini mkataba wa ujenzi wa miradi hiyo minne ulishuhudiwa na Rais John Magufuli Septemba 3, 2018 jijini Mwanza.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli Tanzania (MSCL), Erick Hamissi amesema kutokana na ukarabati ambao umeshaanza kufanyika katika meli za Mv Victoria na Mv Butiama wanaamini kufikia Machi mwaka 2020 ziweze kuanza safari wakati meli mpya ikiwa kwenye hatua za umaliziaji.