Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama imetembelea jengo la kituo cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linalojengwa kwa thamani ya shilingi Bilioni 1.9 katika Mji wa Serikali Mtumba mkoani Dodoma.
Akizungumza baada ya kutembelea mradi huo Mwenyekiti wa Kamati hiyo Vita Kawawa amesema wameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho ambapo amepongeza mradi huo kwa kuzingatia mambo muhimu kwa mahitaji ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kisima kikubwa cha maji na uwepo la tenki la akiba la kuhifadhi maji la lita 150,000.
Akitoa tarifa ya ujenzi wa jengo hilo, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji John Masunga amesema ujenzi huo ulioanza mwezi Aprili mwaka huu na ambao unagharamiwa na fedha za Serikali, umefikia asilimia 50.53 huku ukitumia asilimia 34.24 ya fedha zilizotolewa.