Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ujenzi daraja la Sibiti wakamilika

5da3dfdf549478a13a16b760a27da721 Ujenzi daraja la Sibiti wakamilika

Thu, 17 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kazi ya ujenzi wa daraja la Sibiti imekamilika.

Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Mwanhuzi, wilayani Meatu, mkoani Simiyu kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya stendi ya Mwanhuzi.

"Nimepita pale darajani leo na kukagua ujenzi, kazi imekamilika yaliyobakia ni matengenezo madogo na kuboresha mapito ya mifugo ambayo yamejengwa chini ya daraja kwa pembeni ili iweze kwenda ng'ambo ya pili kupata maji bila kupita juu ya daraja," alisema.

Alisema Serikali ilipoanza kujenga barabara, ilianza kuunganisha mikoa kwa mikoa na sasa tuko kwenye uunganisha wilaya kwa wilaya kwa kiwango cha lami.

"Hapa Meatu tuna barabara ya kutoka Busega hadi Bariadi kupitia Maswa na Shinyanga ambayo inaunganisha pia mikoa ya Shinyanga na Simiyu lakini pia inaunganisha wilaya za Maswa na Meatu."alisema na kuongeza;

"Lakini daraja nililolikagua leo (jana) linapitiwa na barabara ya kutoka Bariadi-Meatu-Mkalama (pale Gumanga) na inaenda kuuunganisha na Singida Vijijini pale Iguguno. Barabara hii iko kwenye Ilani ya CCM Ukurasa 75 na inasomeka Bariadi-Kisesa-Mwandoya-Ngoboko-Mwanhuzi-Sibiti-Mkalama-Iguguno."

Alisema, barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 289 ambayo itajengwa kwa kiwango cha lami inaunganisha wilaya za Bariadi na Meatu, Meatu na Mkalama, na Mkalama na Singida Vijijini.

"Hili daraja limeisha na kazi iliyobakia ni ya kuweka lami kilometa 17 kutoka darajani kuelekea Mkalama na kilometa nane kutoka darajani kuelekea Meatu."

Alisema maboresho ya miundombinu yanayofanyika nchini yanamuwezesha Mtanzania achague aina gani ya usafiri atumie pindi akitaka kwenda mahali.

"Maboresho haya yatamsaidia Mtanzania akitaka kusafiri aamue mwenyewe anataka atumie usafiri gani. Reli zimefufuliwa na mpya zinajengwa, meli zinajengwa, ndege zimeshanunuliwa japokuwa wanazisema lakini wanazipanda."alisema.

Alitumia fursa hiyo kumuombea kura mgombea urais kupitia CCM, John Magufuli, mgombea ubunge wa jimbo la Meatu, Leah Komanya na mgombea udiwani kata ya Mwanhuzi, Igupuli Gambanabi.

Katika hatua nyingine, aliyekuwa mbunge wa Meatu, Juma Salum alisema anawaunga mkono wagombea waliopitishwa na CCM na wala hajawatuma watu waseme vinginevyo.

"Kuna watu wanapitapita huko na wanatumia jina langu, wanasema nimewatuma. Naomba mnikome sababu situmiki hivyo. Nawaombeni sana wale wafuasi wangu tumuunge mkono Leah Komanya kwani ndiye aliyepitishwa na Chama cha Mapinduzi," alisema Salum na kuongeza;

"Ninaomba kura zetu zote tumpe Dk John Pombe Magufuli. Tumwoneshe shukrani zetu kwa mambo mazuri aliyotufanyia wana-Meatu. Leo Waziri Mkuu umepita kwenye daraja ambalo yeye katujengea, tuna kila sababu ya kumshukuru kwa kumpa kura zetu za ndiyo," alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz