Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ujenzi barabara njia 8 Dar- Pwani wafikia 96%

5efe9631ed19375ffff5fa8642e3fc29.png Ujenzi barabara njia 8 Dar- Pwani wafikia 96%

Sat, 28 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

UPANUZI wa barabara ya Morogoro ili kuwa na njia nane kutoka Kimara Dar es Salaam hadi Kibaha mkoani Pwani umefikia asilimia 96.

Ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 19.2, ulizinduliwa na Rais John Magufuli Desemba 19, 2018 na inajengwa na kampuni ya kizalendo ya Estim kwa gharama ya Sh bilioni 141.5.

Mradi huo unaotekelezwa kwa fedha za serikali unakwenda sambamba na ujenzi wa barabara za juu Ubungo kwenye makutano ya Barabara ya Mandela na Sam Nujoma.

Mkurugenzi wa Miradi wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Chrispianus Ako alilieleza gazeti hili jana kuwa upanuzi wa barabara hiyo utakamilika Januari mwakani.

Kuhusu barabara za juu Ubungo, Ako alisema zimekamilika kwa asilimia 100 na kwamba kazi iliyobaki kwa barabara za chini ni kumalizia kufunga taa za kuongoza magari yanayokwenda upande wa kulia.

Alisema tarehe ya kufunguliwa kwa barabara hizo za juu, jina, na kiongozi atakayezifungua, itapangwa na serikali.

Wakati akizindua upanuzi wa barabara ya Kimara-Kibaha, Rais Magufuli alisema ifikapo mwaka 2030, Jiji la Dar es Salaam litakuwa miongoni mwa majiji matano makubwa barani Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya watu zaidi ya milioni 10.

Majiji mengine aliyoyataja ni Cairo nchini Misri, Luanda nchini Angola, na Lagos nchini Nigeria.

Wakati wa uzinduzi wa ujenzi huo aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, alisema upanuzi unaofanywa ni muhimu kwa kuwa barabara hiyo inaunganisha shoroba kuu mbili ikiwemo ya kati inayoanzia Dar es Salaam na kupitia mikoa ya Morogoro, Dodoma, Singida, Shinyanga na kuunganisha nchi za Burundi, Uganda na Rwanda.

Aliitaja shoroba nyingine kuwa inaanzia Dar es Salaam na kuunganisha nchi za Zambia, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Kutokana na umuhimu wa barabara hiyo ambayo awali ilikuwa na njia mbili, Kamwelwe alisema imepewa jina la ‘Tanzania One’.

Alisema kabla ya upanuzi barabara hiyo ilikuwa na uwezo wa kupitisha magari 50,000 kwa siku, lakini ikijumuishwa na pikipiki na bajaji inafanya jumla vya vyombo vyote vya moto vinavyopita hapo kwa siku kuwa 70,000.

Chanzo: habarileo.co.tz