Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ujenzi SGR Kwala wafikia 90%

C0b489726c63eccc9ab3919649f80557 Ujenzi SGR

Tue, 28 Sep 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

UJENZI wa reli ya kisasa (SGR) katika eneo la Kwala mkoani Pwani, umefikia zaidi ya asilimia 90 huku Watanzania wakijivunia kupata ujuzi utakaowawezesha kufanya kazi mahali popote ndani na nje ya nchi.

Kwa mujibu wa msimamizi wa Mradi Kwala hadi Ngerengere wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Kelvin Kimambo, eneo hilo litaanza kutumika mwishoni mwa mwaka huu kama ilivyopangwa kwani shughuli zote za ujenzi ziko kwenye hitimisho.

"Kazi nyingi zimefanywa na Watanzania katika miundombinu yote iliyopo hapa ambayo baadhi yake ni karakana za vichwa vya treni na mabehewa, ghala, jengo la ofisi kuu na la kuoshea treni," alisema.

Mingine ni jengo la mafuta na mchanga, la kuhifadhi bidhaa hatarishi (mionzi ya nyuklia), tangi la maji na jengo la zimamoto pamoja na la madereva kubadilishia nguo.

Alisema kumalizika kwa mradi huo kutaleta mabadiliko katika sekta nyingi, ikiwemo kuondoa mrundikano wa mizigo bandarini kutokana na uwepo wa treni za kuisafirisha kwa mwendokasi kutoka bandarini hadi Kwala.

HabariLEO ilishuhudia baadhi ya majengo yakiwa yamekwishafungwa mitambo yote na vijana wa kitanzania kupitia kandarasi ndogo, likiwemo jengo la zimamoto na karakana ya mabehewa.

Katika karakana hiyo, vijana kupitia kandarasi ndogo ya Kampuni ya Magare inayojishughulisha na uhandisi wa umeme, walikutwa wakimalizia kufunga mitambo ya kupeleka hewa chafu nje na ya kuingiza hewa safi ndani.

Mmoja wa vijana hao, Alphan Lumando, alisema mbali na mitambo ya hewa safi na chafu, tayari ameshajifunza kuendesha mitambo kadhaa licha ya kwamba alijiunga na Kampuni ya Magare mara baada ya kumaliza kidato cha nne akiwa hana ujuzi wa aina yoyote.

Msimamizi vijana hao, Mwinyi Ahmed, alisema baada ya kuona vijana wengi wanakuwa wepesi wa kujifunza mambo mbalimbali, Kampuni ya Magare imepanga kuwapeleka vyuo vya ufundi stadi kulingana na ujuzi wa mtu, ili wasome rasmi na kupata vyeti vitakavyowawezesha kufanya kazi mahali popote.

Chanzo: www.habarileo.co.tz