Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uhamisho wakumba majaji watatu, mahakimu watano

14042 Pic+majaji TanzaniaWeb

Mon, 27 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Majaji watatu wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha akiwapo Salma Maghimbi aliyesikiliza kesi ya mauaji ya Bilionea Msuya, naibu msajili na mahakimu watano wamehamishwa mkoani hapa.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama Mkoa wa Arusha, Edward Mbara alitoa taarifa hiyo juzi katika hafla ya kuwaaga iliyofanyika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).

Mbara aliwataja wengine waliohamishwa ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Sekela Mushi na Dk Modesta Upiyo.

Jaji Mushi anakwenda Songea kuendelea na wadhifa huo, Maghimbi amehamishiwa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi Dar es Salaam na Dk Upiyo amehamishiwa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga.

Mbara alisema majaji wanaochukua nafasi zao Moses Mzuna anayekuwa mfawidhi Kanda ya Arusha akitokea Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi Dar es Salaam.

Majaji wengine waliohamishiwa Arusha ni Issa Maige anayetoka Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza na Thadeo Mwenempanzi ambaye aliteuliwa hivi karibuni. Alisema uhamisho huo ni wa kawaida.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Jaji Nsekela alishukuru kwa ushirikiano waliopewa tangu kuhamishiwa Arusha na kuahidi kuendelea kutenda haki waendako.

Naye mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) mkoani hapa na Manyara, Bariki Maeda alisema mawakili walikuwa wanafanyakazi vizuri na majaji na mahakimu waliohamishwa.

“Tunawaomba muendako muendelee kutenda haki kwa kuwa ni faida kubwa kwa taifa,” alisema.

Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa Arusha, Mrisho Gambo, mkuu wa wilaya Arusha, Gabriel Daqaro aliwataka majaji na mahakimu kusaidia kumaliza kwa wakati kesi za unyanyasaji wanawake na watoto.

Chanzo: mwananchi.co.tz