Handeni. Wakati Mbunge wa Jimbo la Handeni Vijijini Mboni Muhita akisema jimbo lake linakabiliwa na upungufu wa walimu 607 wa shule za msingi, Mbunge wa Handeni Mjini Omary Kigoda amesema uhaba kwenye jimbo lake ni walimu 150.
Mboni amesema sera ya elimu inaelekeza uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 40, uwiano uliopo Handeni vijijini ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi 60.
Wabunge hao walikuwa wakizungumza katika maadhimisho ya Juma la Elimu linaloendeshwa na Mtandao wa Elimu Tanzania (TENMET) katika wilaya ya Handeni.
Mboni amesema anatamani siku moja kuona Wilaya ya Handeni ikiwa kinara wa ufaulu nchini, lakini upungufu huo wa walimu unatishia ndoto hiyo.
"Changamoto nyingine ni uhaba wa miundombinu kama madarasa, nyumba za walimu na vyoo hivyo tunaomba Serikali itazame sekta hii jimboni kwangu," amesema Mboni.
Amewapongeza walimu kwa kuendelea kufundisha kwa bidii licha ya kuwepo kwa changamoto hizo jambo lililosaidia kuongeza ufaulu.
Pia Soma
- Kilo 400 za nyama zilizoharibika zateketezwa Arusha
- TPDC yaomba kupunguziwa mzigo wa Deni la Serikali
- TPDC yabaini viashiria vya mafuta nchini
Kutokana na changamoto hizo Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia sekta ya elimu Tixon Nzunda ameziagiza wilaya hiyo kuondoa uhaba wa walimu kwa kuwahamisha walimu wa sekondari.
Amesema wakati shule za msingi zikikabiliwa na uhaba wa walimu shule za sekondari zina ziada ya walimu 10,000 wa masomo ya sanaa.