Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uhaba wa maji unavyowatesa Same

MRADI MAJI Uhaba wa maji unavyowatesa Same

Tue, 27 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakazi wa Same mjini mkoani Kilimanjaro wamelalamikia ukosefu wa huduma ya majisafi na salama ya bomba, hali inayowafanya kutumia gharama kubwa kuyanunua kwa watu waliochimba visima.

Kilio hicho cha maji kimetolewa leo Jumatatu Februari 26, 2024 mbele ya Kamati ya Utekelezaji ya Umoja wa Vijana ya Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa ikiongozwa na makamu mwenyekiti wa umoja huo, Rehema Zombi wakati wa ziara wilayani Same.

Changamoto ya maji ilianza kuibuliwa katika Shule ya Sekondari ya Same baada ya makamu mwenyekiti huyo kufika shuleni hapo kisha wanafunzi kumlalamikia kukabiliwa na uhaba wa maji hali inayowafanya washindwe kuoga.

Upatikanaji wa maji Same kwa sasa ni asilimia 76, huku Kata ya Same Mjini yenye wakazi takribani 22,000, ikitajwa kuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa huduma hiyo na sasa wanasubiri kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe.

Wakati msafara wa kamati ya utekekezaji ulipowasili shuleni hapo, walisimamishwa baadhi ya viongozi kusalimia na alipoitwa mkuu wa wilaya hiyo, Kasilda Mgeni, wanafunzi walipaza sauti wakisema hawaogi.

Mbali na wanafunzi hao, pia katika mkutano wa hadhara uliofanyika stendi ya mabasi Same mjini, wananchi wameeleza kuwa, changamoto ya maji katika maeneo hayo ni kubwa hali inayowafanya, kutumia maji ya visima kwa gharama kubwa huku mengine yakiwa si salama.

Mkazi wa eneo hilo, Hassan Mkubwa amesema maji ya bomba wanayasikia kwa wenzao na ya visima wanayoyategemea si salama kwa kuwa baadhi ya maeneo yanatumiwa na mifugo wakiwamo mbwa.

"Sisi majisafi tunayasikia kwa wenzetu, kwa sasa tunatumia maji ya visima tunayoshirikiana na mifugo na mbwa, hii ni changamoto kubwa na ya muda mrefu, tunaomba msikie kilio chetu."

Mkazi mwingine wa Same, Ashura Mgonja amesema kwa sasa wananunua maji ndoo moja kwa Sh300, gharama ambayo ni kubwa na wananchi wengi hawawezi kuimudu.

"Kwa hapa Same Mjini, wapo watu wanaenda kununua maji kwa waliochimba visima halafu wanakuja kutuuzia kwa Sh300 kwa ndoo moja, tunaomba Serikali iangalie hili, changamoto hii imekuwa mwiba kwetu," amesema Ashura.

"Wauzaji hawa wa maji wao wananunua ndoo moja Sh100 kukiwa na umeme, lakini katika kipindi hiki cha changamoto ya kukatika umeme, wanauziwa Sh150 na wakileta huku wanatuuzia Sh300 ili kupata nao faida."

Hata hivyo, mkuu wa wilaya hiyo, Mgeni amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na akisema Serikali inaendelea kukamilisha mradi mkubwa wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe na ifikapo Juni mwaka huu, awamu ya kwanza itakuwa imekamilika na Same Mjini wataanza kupata maji.

"Ni kweli, Same tuna matatizo makubwa ya maji hasa katika eneo hili la mjini, lakini tayari mradi mkubwa wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe, umefikia hatua nzuri na Juni awamu ya kwanza itakuwa imekamilika na Same Mjini watapata maji."

Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Sombi amesema chama kitaendekea kuisimamia Serikali ili kuhakikisha huduma hiyo muhimu inapatikana na wananchi wanaondokana na changamoto hiyo.

"Nimesikia changamoto ya maji Same na changamoto hii nimeisikia pia kwa wanafunzi, Serikali imeahidi kushughulikia hili na sisi kama chama tutaendelea kusimamia ili kuhakikisha changamoto hii inamalizika,” amesema Sombi.

Kamati ya utekelezaji ya UVCCM Taifa, ipo katika ziara mkoani Kilimanjaro lengo likiwa ni kuangalia uhai wa chama na jumuiya zake pamoja na kukagua miradi ya maendeleo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live