Upungufu wa matundu ya vyoo katika shule za sekondari na msingi Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro kumetajwa kuchangia watoto wengi wa kike kushindwa kuhudhuria masomo katika kipindi cha hedhi.
Hayo yamebainishwa na Ofisa Miradi wa Shirika la Ongawa lililopo wilayani humo, Leonia Andrew wakati shirika hilo kwa kushirikiana na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) walipotoa mafunzo ya kuwajengea wanajamii uelewa juu ya utengwaji wa rasilimali zinazozingatia usawa wa kijinsia.
Leonia amesema Shirika la Ongawa limekuwa na mradi wa jinsia na hedhi katika kata za Kalimawe, Lugulu na Kihurio wilayani humo na changamoto kubwa waliyoibaini kuwa kikwazo kwa watoto wa kike kipindi cha hedhi ni upungufu wa matundu ya vyoo shuleni, pamoja na ukosefu wa maji na vyumba maalumu kwa ajili ya watoto wa kike kujisitiri.
Amesema pamoja na changamoto hiyo katika jamii masuala ya hedhi hayajaingizwa kwenye mipango kazi na bajeti jambo ambalo limewasukuma kuanza kuhamasisha jamii ili ione umuhimu wa kuingiza masuala hayo kwenye mipango kuanzia ngazi za vijiji.
"Moja ya changamoto tuliyoiona ni upungufu wa matundu ya vyoo na hakuna vyumba maalumu vya watoto wa kike kujisitiri wakati wa hedhi, hivyo Ongawa kwa kushirikiana na TGNP, tunaihamasisha jamii kuona umuhimu wa kutenga bajeti kwa ajili ya kukabiliana na changamoto hii"
Ameongeza kuwa "Kumekuwepo na utoro shuleni, kwani mabinti wengi hawawezi kuhudhuria vipindi vyote shuleni wakati wakiwa kwenye hedhi hivyo kuna umuhimu wa kujengwa kwa vyumba vya kujisitiri ili kuondokana na ile adha ya wao kutoroka au kushindwa kuhudhuria vipindi vyote na kuchangia kuanguka kitaaluma"
Advertisement Ofisa idara ya utafiti, uchambuzi na maarifa kutoka TGNP, Speratus Kyaruzi amesema wametoa mafunzo hayo kutokana na uwepo wa changamoto kubwa ya kutotekelezeka kwa miradi mingi ikiwemo ya maji, elimu, afya na sekta nyingine zinazogusa wanawake na wanajamii wengine kwa ujumla.
"Ufike wakati wa wanajamii kushiriki katika maandalizi ya bajeti ambayo ipo katika mrengo wa kijinsia na wanawake washiriki katika mipango hiyo ili waweze kusema malengo na mahitaji yao na kutengwe rasilimali fedha kwenye bajeti kwa ajili ya kukidhi hayo mahitaji"