Zipo dalili za wazi za upungufu wa chakula cha asili mkoani Kagera unaotokana na sababu mbalimbali za kimazingira, zikiwemo zinazohusishwa na mabadiliko ya tabianchi.
Moja ya sababu hizo ni ugonjwa usio na tiba wa mnyauko (Banana Xanthomonas Wilt). Ugonjwa huu umeathiri migomba kwa kiwango kikubwa na kusababisha uzalishaji wa ndizi kupungua.
Hali hiyo, kwa mujibu wa wenyeji wa mkoa huo, imebadili utamaduni wa matumizi ya chakula hicho cha asili, wengi wameanza kutumia vyakula mbadala.
Pamoja na tatizo hilo, mkoani Kagera kwa sasa hakuna mashamba mapya yanayoanzishwa, huku baadhi ya wakulima wakiwa wamekata tamaa kutokana na maradhi hayo. Ugonjwa wa ajabu waibuka, wafananishwa na Ukimwi, Mbunge atoa tahadhari
Ni nadra kukuta kilimo cha umwagiliaji wa migomba, badala yake zao hilo hutegemea majira ya mvua, ambazo kwa sasa hazitabiriki kama ilivyokuwa zamani na wenyeji wanaamini zinaponyesha baada ya ukame mrefu, ndipo mnyauko unaonekana zaidi.
Mkazi wa Kijiji cha Ihunga, Wilaya ya Muleba, Rudovic Mwebesa anasema miaka 10 iliyopita alikuwa miongoni mwa wauzaji wakubwa wa ndizi, lakini mashamba yake yalishambuliwa na mnyauko ambao kwa kiasi kikubwa uliathiri uzalishaji ndizi.
Anasema awali alishauriwa kuteketeza migomba yote na kupanda upya kama njia ya kupambana na mnyauko na akafanya hivyo. Katika kipindi hicho, ilimlazimu kubadili utamaduni wa kutegemea ndizi pekee kwa chakula na chanzo cha mapato.
Hata hivyo, miaka miwili baadaye mashamba yake yalishambuliwa tena na ugonjwa uleule, hali iliyomkatisha tamaa kuendelea na kilimo hicho.
“Nililazimika kubadili aina ya kilimo baada ya mashamba yangu mawili kushambuliwa na ugonjwa wa mnyauko. Awali, nilikuwa miongoni mwa wauzaji wakubwa wa ndizi kabla ya kuingia kwa janga la ugonjwa wa migomba,” anasema.
Maelezo ya Mwebesa hayaachani sana na ya Deus Patrick, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Buhanga, Kata ya Buganguzi wilayani humo, anayesema ugonjwa wa mnyauko umesababisha wananchi wengi kukosa uhakika wa chakula kwa kuwa mashamba yao ya migomba si ya kutegemea sana kama zamani.
Anasema hata kwenye vikundi vya ujima katika eneo lake ambavyo zamani vilitoa huduma ya ndizi wakati wa misiba, vililazimika kubadili utaratibu na kuruhusu huduma vya vyakula vingine kama ugali na wali kwa kuwa ndizi zilianza kuwa adimu.
Anahusisha hali hiyo na mabadiliko ya tabianchi, aliyosema yameathiri hata uzalishaji wa ndizi na upatikanaji wake.
Kwa uzoefu wake, anasema ugonjwa wa mnyauko unasambaa sana wakati wa mvua ikilinganishwa na wakati wa kiangazi, suala ambalo pia linaungwa mkono na Charles Mwijage, Mbunge wa Muleba Kaskazini ambaye pia ni mkulima maarufu wa migomba.
Mwijage katika mahojiano na Mwananchi, anasema upo uhusiano mkubwa kati ya mnyauko na mabadiliko ya tabianchi.
“Linapotokea jua kali, likiisha ndipo mnyauko unakuwa mkali, kwa hiyo kuna mahusiano,” anasema Mwijage.
Anatoa mfano wa kipindi cha mwishoni mwa Desemba 2023 na Januari 2024 kuwa mnyauko unazidi kukolea kwa kuwa hapo awali kiangazi kilikuwa kimekolea sana.
“Mfano mimi katika mashamba yangu kwa wiki moja ya kuanzia Desemba 25 nimeng’oa migomba 60 yenye mnyauko. Unaweza kuona hapo, ugonjwa huu unapunguza production (uzalishaji) ya ndizi kwa kiwango kikubwa,” anasema.
Akiungana na Mwijage, mtaalamu wa kilimo Agripina Mutalemwa anasema ugonjwa huo ni tatizo kubwa katika maeneo mengi ya Mkoa wa Kagera na udhibiti wake bado unasuasua.
Mutalemwa ambaye ni ofisa ugani mstaafu, anasema ugonjwa huo unazidi kusambaa kutokana na baadhi ya wakulima kukosa zana za kuharibu migomba yenye ugonjwa, badala yake kuazima chache walizonazo wenzao.
“Kuna tatizo la umasikini, watu wana mashamba lakini hawana vifaa kama panga na ekiosho (chimbuo la kungolea migomba) na vingine, wanaazimana na kusambaza ugonjwa,” anasema Mutalemwa maarufu Bibi Shamba, mkazi wa Kijiji cha Irogelo, Kata ya Kamachumu.
Kutokana na hali hiyo, Patrick anashauri uwepo utaratibu wa kuwasaidia wakulima kukagua na kubaini migomba iliyoathirika na baada ya kuitambua washauriwe hatua za kuchukua ili ugonjwa huo usiendelee kusambaa kwenye mashamba mengine.
Katika hilo, Mwijage anapendekeza uwepo usimamizi wa mashamba na ukaguzi wa kila wakati, ili dalili zikibainika mgomba wenye tatizo uharibiwe kabla ya kuambukiza mingine.
Vilevile anasisitiza, “Serikali ichukue hatua madhubuti kudhibiti mnyauko, ikiwa ni pamoja na kuweka adhabu kwa watu wanaokaidi kuharibu migomba yenye matatizo.
Mbunge huyo anatoa mfano wa Uganda na Rwanda ambako anasema adhabu zimesaidia kudhibiti tatizo hilo.
Hofu kubwa
Ndizi likiwa zao kuu la chakula na biashara, kwa miaka mingi limeshika uchumi wa wakazi wengi wa Mkoa wa Kagera, sawa na kahawa. Hofu kubwa iliyopo sasa ni tishio la zao hilo kutoweka baada ya kushambuliwa na mnyauko na magonjwa mengine yanayoshusha uzalishaji.
Kulingana na Mwijage, madhara ya moja kwa moja ya mnyauko ni uzalishaji wa ndizi kupungua baada ya migomba kudhoofu, matunda yake kupungua au kuharibika kabisa.
Anasema ndizi na kahawa vinashindana katika kuingiza fedha kwenye familia, hivyo kupungua kwa uzalishaji wake, matokeo yake ni upungufu wa chakula na chanzo cha mapato, mambo ambayo hatimaye yanasababisha tatizo la lishe.
Si mnyauko pekee
Licha ya tatizo hilo ambalo limeshika kasi, yapo magonjwa mengine yanayotajwa kusumbua wakulima wa zao hilo mkoani Kagera, ambayo ni fuzari na sigatoka.
Magonjwa hayo yanaufanya mgomba kuwa na madoa, unyanjano na kuvu. Kuenea kwake kunahusishwa pia na mabadiliko ya tabianchi.
Gabriel Lukosi, ofisa kilimo kitengo cha uhaulishaji wa teknolojia katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Maruku (Tari), anasema magonjwa mengi ya migomba, ukiwemo mnyauko, yanasababisha ndizi kuiva kabla ya kukomaa, majani kubadilika rangi, shina kutoa utomvu wa njano na mwisho wa yote ni kupungua kwa mavuno kwenye mashamba ya wakulima.
Lukosi anasema baadhi ya magonjwa hayo yanasambaa kutegemeana na mabadiliko ya hali ya hewa, hasa ugonjwa wa sigatoka, unaosababisha mgomba kuwa na madoa.
Anashauri wakulima kutumia miche salama iliyofanyiwa utafiti ili kupata mavuno bora, huku wakisafisha mashamba kwa vifaa safi, kama njia ya kupambana na magonjwa.
Mtafiti huyo anawakumbusha wakulima kuacha mazoea ya kushirikiana vifaa vya shambani kwa kuwa ni njia ya kueneza magonjwa na kuwa, baada ya migomba iliyoathirika kuteketezwa, shamba linatakwa kukaa miezi minne hadi sita bila kutumika.
Naye Utoni Nkokelo, mtafiti katika Kitengo cha Uhaulishaji wa Teknolojia katika kituo hicho, anasema mabadiliko ya tabianchi yamechangia kuibuka kwa magonjwa mapya, hali inayoongeza hofu kuhusu usalama wa chakula kinachotokana na ndizi.
“Hata ukame ni matokeo ya mabadiliko ya tabianchi, kuna magonjwa mapya ya migomba yameibuka kama ule wa kufifia kwa ncha za majani (Banana bunchy top virus) na unatajwa kuwa hatari zaidi kwa kuwa unashambulia migomba ya aina zote,” anasema.
Nkokelo anasema ugonjwa huo umegundulika pia katika mashamba ya wakulima wa migomba mkoani Kigoma na hauna tiba, sawa na ilivyo mnyauko.
Anawataka wakulima kuchukua tahadhari kwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu.
Yanaathiri uchumi
Kwa ujumla, Nkokelo anasema magonjwa ya migomba yanaathiri uchumi kuanzia kwenye kaya hadi Taifa kwa kuwa mavuno yatapungua, hivyo kipato kupungua.
Mbaya zaidi, anasema hali hiyo inatokea wakati wananchi wengi wa Mkoa wa Kagera bado wanategemea ndizi kama zao la chakula na biashara, licha ya changamoto zilizopo.
Akizungumzia ubora na usalama wa mbegu za migomba, Nkokelo anasema moja ya changamoto ni kituo cha utafiti kushindwa kukidhi wingi na ubora wa mbegu kulingana na ukubwa wa mahitaji.
Anasema ujenzi wa maabara katika kituo hicho unaweza kuongeza upatikanaji wa miche bora ya migomba na iliyo salama.
Hali si shwari
Akizungumzia hali ilivyo mkoani Kagera na kwingineko kuhusu migomba, Mtafiti Mwandamizi wa zao hilo nchini, Dk Mpoki Shimwelaanaonya mkoa huo hauko salama baada ya kuibuka kwa magonjwa mengi yanayoathi uzalishaji wa zao hilo.
Amesema baadhi ya magonjwa yameingia nchini kutokea mataifa jirani ya Rwanda, Burundi, DR Congo na Uganda kutokana na utamaduni wa wakulima kugawiana mbegu, hivyo kuwa chanzo cha kusambaa kwa magonjwa.
Kutokana na hali hiyo amesema Mkoa wa Kagera ambao umezungukwa na nchi ambazo migomba imeshambuliwa, hauko salama kwa kuwa wananchi wanaendelea na mazoea ya kugawiana mbegu bila tahadhari.
Kwa mujibu wa Dk Shimwela, kusambaa kwa magonjwa ya migomba kunahusiana na mabadiliko ya tabianchi, ikiwa ni pamoja na kubadilika kwa tabia za bakteria na wadudu wengine ili waweze kukabiliana na mabadiliko yanayotokea.
"Kutokana na mabadiliko ya tabia nchi wadudu nao wanabadilika, kama walikuwa hawawezi kufanya jambo fulani, sasa wanaweza kulifanya. Mfano bungua wa mgomba zamani walishambulia baadhi tu ya migomba, lakini leo wamebadilika wanashambulia aina zote," anasema Dk Shimwela, mkuu wa Kituo cha Utafiti Maruku mkoani Kagera.
Mtafiti huyo na mratibu wa zao la ndizi nchini, anasema zipo sababu za kisanyansi zinazosababisha kuongezeka kwa wadudu ambao wanashambulia migomba kwa kasi.
"Kuna ongezeko la wadudu hatarishi wa migomba, zamani walikuwa wachache sana. Sasa wameongezeka na matokeo yake wanashambulia ndizi ambazo awali zilikuwa salama," anasema Dk Shimwela.
Akitoa mfano, anasema hali hiyo imesababisha kushambuliwa kwa migomba aina ya Fia ambayo ilikuwa na uwezo mkubwa wa ukinzani wa magonjwa na hali ya mabadiliko ya tabianchi inayotokea leo.
Anakumbusha kuwa hali hiyo inaongeza hofu ya kutokuwa na uhakika wa chakula kwa wananchi na hata uchumi kuathirika kwa kuwa zao la ndizi linategemewa kwa chakula na biashara.
Wilaya ya Karagwe, ikipakana na Uganda na Rwanda, kama zilivyo nyingine, ipo katika tishio hilo baada ya migomba kushambuliwa na magonjwa.
Hata hivyo Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa wilaya hiyo, Adam Salum anasema pamoja na hofu iliyopo wilaya imeimarisha mikakati ya kuelimisha wakulima kupambana na magonjwa ya migomba.
Anasema pamoja na kuwa hakuna pengo la moja kwa moja la upungufu wa chakula, tatizo hilo liko wazi kwenye mashamba ya wakulima wa migomba katika wilaya hiyo.
"Katika Wilaya ya Karagwe zao kuu la chakula ni ndizi, ni ukanda unaozalisha zao hilo kwa wingi, ili kupambana na changamoto ya magonjwa tuliunda vikundi vya kung'oa na kuteketeza migomba iliyoshambuliwa na kupiga marufuku uingizaji wa mbegu za migomba kutoka nje ya wilaya na nchi jirani," anasema Salum.
Zaidi kuhusu ugonjwa
Ugonjwa wa mnyauko (Banana Xanthomonas Wilt) umepewa jina kutokana na bakteria wanaoambukiza na hatimaye kuua mgomba. Ugonjwa huo umeongezeka nchini Tanzania tangu mwaka 2006 mkoani Kagera ukitokea Uganda.
Ugonjwa huu hushambulia aina zote za migomba na matokeo ya utafiti yameonyesha uwezekano wa kupatikana aina sugu siku zijazo.
Ingawa haujapata dawa, udhibiti wake ni pamoja na kupanda mazao mapya yasiyo na ugonjwa, kutumia zana safi za kukatia na kuondoa maua dume ili kupunguza kuathiriwa kupitia wadudu wanaobeba bakteria katika utomvu.
Ugonjwa huu husababisha majani ya migomba kuwa ya njano na kisha kunyauka na kukauka. Pia huathiri matunda ya ndizi, shina la mgomba kuoza na hatimaye kufa.
Ugonjwa huu ulianzia Uganda na kusambaa Tanzania, Kenya, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia Congo.
Katika nchi hizo uligundulika kwa vipindi tofauti, na hivi sasa upo katika nchi zote za Afrika Mashariki na Kati.
Januari 2006 mnyauko uligundulika katika Kijiji cha Kabale kilichopo tarafa ya Izigo, Wilaya ya Muleba na hadi Juni 2012 ulikuwa umeenea wilaya mbalimbali za mkoa huo.
Maeneo mengingine ya Tanzania ugojwa ulithibitishwa Tarime, Chato, Geita, na wilaya kadhaa za mkoani Kigoma, Ukerewe na Mwanza.
Ugonjwa huo huenea kutoka mmea hadi mmea au shamba hadi shamba kwa njia ya viumbe kama vile ndege, nyuki, binadamu, ngedere na tumbili; au kupitia zana za kufanyia kazi shambani kama vile panga, chezo, chimbuo, visu na nyengo (mundu).