Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ugonjwa wa ajabu waua Mifugo Arusha

Mifugo Arushaaaaa Ugonjwa wa ajabu waua Mifugo Arusha

Mon, 4 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ugonjwa wa ajabu unaoathiri afya ya mifugo na kusababisha vifo kwa haraka, umeibuka katika baadhi ya vijiji mkoani Arusha, huku jamii ya wafugaji ikiomba serikali ifanye utafiti wa kubaini chanzo cha ugonjwa huo.

Baadhi ya wafugaji kutoka Wilaya ya Longido, wanadai ugonjwa huo unakumba mifugo, hasa mbuzi na kondoo, na huathiri ubongo kwa kasi hadi kusababisha vifo vingi.

Taarifa kuhusu ugonjwa huo, ilitolewa na mmoja wa wafugaji wa Wilaya ya Longido, Nambori Nabaki, mwishoni mwa wiki wakati wa jukwaa maalum lililokutanisha wadau wa kilimo ikolojia, chini ya mwavuli wa shirika lisilo la kiserikali la Island of Peace.

Akifafanua zaidi kuhusu ugonjwa huo, ambao kabila la Kimasai wameubatiza jina la ‘Ormilo’ Nabaki, amesema kama usipodhibitiwa kwa haraka unaweza kusababisha jamii ya wafugaji kuwa maskini katika kipindi kifupi, kwa kuwa unaenezwa na vimelea.

"Mbuzi na kondoo kule kwetu (Longido), wanakwisha kwa ugonjwa wa Ormilo. Tumejaribu kuwachinja mbuzi na kondoo kuangalia tatizo ni nini baada ya kuanguka na kufa,” amesema.

Amesema mifugo iliyopata ugonjwa huo ikichingwa ubongo wao unakuwa kumejaa maji na kuiomba serikali ifanye utafiti na ipeleke wataalamu kwa ajili ya kunusuru mifugo iliyobaki isiendelee kufa.

Amesema licha ya mifugo hiyo kufa kwa ugonjwa huo tishio, bado wanakabiliana na changamoto ya uwapo wa magugu vamizi katika maeneo ya malisho yanayozuia majani ya kulishia mifugo kuota.

Kwa mujibu wa Daktari wa Mifugo wa Halmashauri ya Arusha, Linus Prosper, ugonjwa huo wa Ormilo, huwapata zaidi wanyama aina ya mbuzi, kondoo na mbwa.

Dk. Linus, ameeleza kuwa ugonjwa huo chanzo chake unatokea kwenye utumbo wa mbwa, ambapo akijisaidia kwenye majani na yakaliwa na mbuzi na kondoo, ndiko hupata maambukizi.

"Mbwa mwenye minyoo anapojisaidia kwenye majani, na binadamu akakata majani yenye kinyesi akawalisha mifugo, wanakula ile minyoo na ikiingia kwenye mifugo inabadilika kuwa lava. Hivyo, wanazaliana na mbuzi anaanza kuonyesha dalili anakuwa na kizunguzungu mpaka anakufa,” amesema.

Amesema ugonjwa huo hauna dawa, bali kinachotakiwa ni kutibu minyoo kwa mbwa wote wafugwao na wanaozurura, hiyo ndio tiba pekee ya kuzuia ugonjwa huu usizidi kuenea.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live