Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ugonjwa wa ajabu waitesa familia Babati

Ugonjwapiic Data Ugonjwa wa ajabu waitesa familia Babati

Fri, 12 Aug 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Utadhani unatazama filamu ya kutisha; hivyo ndivyo unavyoweza kusema unapofika Kijiji cha Imbilili Juu, Halmashauri ya Mji wa Babati Mkoa wa Manyara na kukutana na familia ya Helena Hungoli (60) yenye watu wawili wanaougua ugonjwa wa ajabu, akiwamo yeye.

Katika familia hiyo, Helena anaishi kwenye kibanda kidogo na ndugu zake wawili na mtoto wake, Safari Gidale (34).

Ukimwona Helena na Safari unaweza kukimbia au kupatwa na hofu kutokana na kuugua ugonjwa wa ajabu na kusababisha ngozi yenye uvimbe kuning’inia katika sehemu za miili yao.

Helena, ambaye ameota ngozi yenye uvimbe na kufunika upande mmoja wa uso wake pamoja na mdomo, akizungumza na gazeti hili nyumbani kwake jana aliiomba Serikali na wasamaria wema kumsaidia, ikiwamo kutambua hasa tatizo linalomkabili kwa zaidi ya miaka 55.

Alisema kwa sasa hawezi kufanya kazi yoyote ya kumuingizia kipato kutokana na kuwa na hali hiyo tangu akiwa mdogo.

“Kila sehemu ya mwili wangu inauma na kwa hali niliyokuwa nayo, inabidi nishinde nyumbani muda wote na sasa nahitaji msaada mkubwa, Serikali na wasamaria wema nisaidieni,” alisema kwa sauti ya chini yenye majonzi.

Alisema ugonjwa huo ulianza mwaka 1964 akiwa na miaka miwili baada ya nyama ndogo kuanza kuota taratibu kichwani na shingoni na amekuwa anakwenda zahanati za kawaida na kuambiwa aende hospitali kubwa anakoshindwa kwenda kutokana na ukata.

“Nyama hizo zilianza kukua kadiri umri wangu ulivyozidi kuwa, ndipo zikawa kubwa na kusababisha hali hiyo hadi hivi sasa nikiwa na mtoto wangu tunateseka,” alisema.

Alisema mwanzoni mwa miaka ya 80 alifanikiwa kuolewa na kuzaa mtoto mmoja wa pekee mwaka 1988, lakini mume wake alifariki dunia na kumuacha yeye na mtoto wake.

Hata hivyo, mtoto wa pekee wa mama huyo, Safari naye amekumbwa na masaibu mengine makubwa, kwani ameota nyama upande wa kushoto wa mwili wake. Ugonjwa huo unamsababishia maumivu na uzito upande mmoja, hali inayomfanya atembee akiwa amepinda na hana wa kumsaidia.

“Tunaiomba Serikali na wasamaria wema wenye uwezo watusaidie tupate matibabu kwa kuwa hivi sasa mimi na mama yangu hatuna msaada wowote ule tunateseka hapa nyumbani,” alisema Safari wakati akizungumza na gazeti hili.

Alisema uvimbe huo ulianza kumtokea kwenye mwili wake tangu akiwa mdogo na kuvimba zaidi kadiri alivyozidi kuwa mkubwa.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Imbilili Juu, Hassai Suleiman alisema hali ya mama huyo iliwaogopesha majirani hadi kumkimbia hivyo kumfanya aishi katika mazingira magumu zaidi.

Suleiman alisema baada ya kuonekana mara kwa mara na wananchi wa eneo hilo, waliwazoea na wakawa wanawatembelea na kuwapa chakula.

“Wanaishi kwenye mazingira magumu mno, hata kupata mlo wa chakula mara tatu kwa siku kama watu wengine inakuwa changamoto kutokana na hali duni ya uchumi,” alisema Suleiman.

Mdogo wa mama huyo, Josephina Hungoli alisema anaona mwanga utaonekana baada ya waandishi wa habari kufika nyumbani kwao Kijiji cha Imbilili Juu.

“Kupitia ninyi waandishi wa habari, tuna matumaini makubwa na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, watatupa msaada wa matibabu ili ndugu zangu wasaidiwe,” alisema Josephina.

Alisema endapo kuna mtu anaweza kuwapa msaada wawasiliane kwa namba 0682 995922 iliyosajiliwa kwa jina la Hemedi Samweli Maganga.

Mmoja wa madaktari wa Mkoa wa Manyara, Joseph Temu akizungumzia ugonjwa huo wa ajabu uliowakumba mama na mtoto, alisema tatizo hilo linatokana na kurithi.

“Hayo yanatokana na maradhi ya kurithi lakini wakifikishwa hospitali wanaweza kupatiwa matibabu,” alisema Dk Temu.

Jirani wa familia hiyo, Elizabeth Ombay alisema walishindwa kushirikiana nao kutokana na jinsi walivyo.

“Tulishindwa kushirikiana nao awali kwa kuwa walikuwa wanaogopesha mno, lakini majirani wengine ambao wameshika dini kidogo waliweza kuzoea hali hiyo na kuanza kuwatembelea,” alisema.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz