Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ugali wa muhogo waua watoto wa familia moja

88336 Pic+ugali Ugali wa muhogo waua watoto wa familia moja

Sat, 14 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Serengeti.Watoto wanne wa familia moja ya kijiji cha Machochwe mkoani Mara wamefariki dunia huku wawili wakinusurika kifo kutokana na kula ugali wa muhogo unaodhaniwa kuwa na sumu.

Ofisa mtendaji wa Kata ya Machochwe, Yohane Ole alisema watoto hao-- Joseph Michael (13), Zablon John (5), Neema Michael (4) na Neema John (3), walifariki Desemba 7.

Mganga mfawidhi wa kituo cha afya cha Machochwe, Joseph Kiberenge alisema jana kuwa watoto hao walikula ugali wa mihogo michanga ambayo haikuandaliwa vizuri, hali ambayo wanahisi ilitengeneza sumu.

“Kutokana na ukosefu wa chakula, walichimba mihogo michanga ya miezi mitano, bahati mbaya haikuvundikwa vizuri kisha wakasaga ukapikwa ugali. Watoto walipata madhara kwa kuwa kinga yao ni ndogo ya kukabiliana na matatizo ikiwa ni tofauti na watu wazima,” alisema Dk Kiberenge.

Awali, watoto wawili waliofikishwa hospitalini hapo walikuwa wakilalamika maumivu makali ya tumbo, kutapika na kuishiwa nguvu.

“Unga na baadhi ya sampuli zao zimepelekwa kwa mkemia mkuu Mwanza ili kujua ni sumu ya aina gani hasa,” alisema.

“Hatujapata majibu, lakini uchunguzi wa awali tulibaini tatizo hilo kutokana na maelezo na kuangalia namna walivyoandaa, maana mihogo haikuvunda akaamua kutwanga ili apate unga wa watoto,” alieleza.

Familia yazungumza

Baba mzazi wa watoto hao, Michael Mnanka hakuwa tayari kuzungumzia kilichotokea kwa madai alikuwa ameandamwa na matatizo mengi.

Lakini mama wa watoto hao, Maria Michael alisema walikuwa hawana uhakika wa kula wakaamua kutengeneza unga wa mihogo hiyo michanga.

“Ukigeuka huku watoto wanalia hawajala kitu, ikanilazimu kusaga unga huo,” alisema Maria huku akilia.

“Familia yetu ya watu 14 tunaishi kwa mlo mmoja kwa siku. Wakati mwingine uji pekee. Siku hiyo nililazimika kusaga udaga kutokana na mihogo michanga ya miezi mitano niliyochimba.

“Nikavundika na kupondaponda kabla haujakauka vizuri ili watoto wapate chakula.

Maria alisema baada ya kula siku hiyo, usiku wa manane watoto walianza kulalamika maumivu makali ya tumbo.

Alisema wakati wanahangaika, aliwapeleka zahanati ya Merenga, ambapo wawili walifia njiani. Waliporudi nyumbani wakakuta wawili wameshakufa pia, huku wawili wakiwa hoi.

“Wakubwa hatukupata madhara isipokuwa hawa wadogo sijui kilichotokea. Kwa ujumla tunakabiliwa na njaa, kwa sababu mazao yetu yanaliwa na tembo, yaliyopo ndiyo hayo hayajakomaa. Nimeomba msaada mpaka nimechoka,” alisema Maria.

Amosi Michael(18), mtoto mwingine wa familia hiyo, alisema hakupata tatizo baada ya kula chakula hicho.

“Wadogo zangu hali yao ilibadilika usiku wa manane na ilituchukua muda kuwapeleka zahanati kutokana na mazingira ya huku na kusababisha vifo. Hawa wengine wawili wanaendelea vizuri,” alisema.

Ofisa kilimo wa Kata ya Machochwe, James Hitler alisema hali ya chakula ndani ya kata hiyo ni mbaya na kwamba ukame na tembo kuwa ndio vitu vilivyochangia hali hiyo.

“Mpaka sasa eka 239 katika kijiji hicho zimeliwa na tembo na wananchi hawajalipwa kifuta machozi,” alisema.

Debe la mahindi limepanda kutoka Sh7,500 hadi Sh19,500, muhogo kutoka Sh5,000 hadi Sh10,500 katika kata hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu alikanusha kuwa hakuna upungufu wa chakula wilayani hapo na kwenye kata hiyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz