Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ufukuaji makaburi Vingunguti wasitishwa kwa muda

Makaburi Pic Data Ufukuaji makaburi Vingunguti wasitishwa kwa muda

Fri, 31 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ufukuaji wa makaburi ya Vingunguti na kuyahamishia eneo la Mwanagati umesitishwa kwa siku nne.

Hayo ymeelezwa leo Desemba 31, 2021 na Ofisa Afya wa Jiji hilo, Reginald Mlay katika mahojiano maalumu na Mwananchi.

Mlay amesema usitishwaji huo umefikiwa baada ya kutokamilika kwa maandalizi kwa ajili ya kufukua makaburi mengine 150 yaliyogundulika katika siku tatu za ufukuaji.

Kazi ya ufukuaji wa makaburi hayo ilianza  Desemba 27 na ilikuwa ikamilike Desemba 29, lakini kutokana na kugundulika kwa mengine 150 wakati kazi hiyo ikiendelea, Jiji liliamua kuongeza muda.

Akiwa katika eneo la tukio juzi, Meya wa Jiji hilo, Omar Kumbilamoto alisema makaburi hayo yaliyoongezeka yalikuwa yamezibwa na kichaka kilichoota eneo la mita kumi kutoka usawa wa mto ambapo shughuli hiyo inapaswa kufanyika na kutokana na hilo alisema wameamua kuongeza siku tatu zaidi.

Hata hivyo Mlay amesema wakati maamuzi ilikuwa iwe hivyo, kazi hiyo jana na leo imeshindwa kufanyika kutokana na kutokamilika kwa maandalizi ikiwemo kutengeneza majeneza.

“Katika kazi hii, kuna maandalizi yanayotakiwa kufanywa kabla na kwa kuwa yaliyoongezeka hayakuwepo kwenye bajeti wala ratiba, hivyo tumesitisha kwanza ili kukamilisha maandalizi yake.

“Pamoja na kusitisha shughuli kwa siku tatu, nawaomba wananchi wanaojua wana miili ya wapendwa wao wayoizika katika eneo hilo kuendelea kujitokeza ofisi ya Serikali ya Mitaa wa Butiama, Kata ya Vinguguti kujiandikisha ili waweze kushiriki nasi,”amesema Mlay.

Uhamishaji wa makaburi hayo, unafanywa baada ya kuendelea kumomonyoka kwa ardhi eneo hilo kunakosababishwa na mafuriko yanayotokea kipindi cha mvua katika mto Msimbazi.

Mpaka sasa zaidi ya makaburi 300 yameshasombwa, huku mengine majeneza yakionekana yakiwa yananing’inia pembezoni mwa  kingo za mto huo na mpaka kufika jana makaburi 238 yalikuwa yameshafukuliwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live