Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Udumavu Kagera wapungua

Da5a0e679db5fa680a9aece3082ab748 Udumavu Kagera wapungua

Thu, 24 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

TAKWIMU za udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano mkoani Kagera zimeendelea kupungua kutoka asilimia 41 hadi 39 mwaka 2019.

Hiyo inatokana na wananchi kuendelea kuwa na mtazamo chanya kuhusu malezi ya watoto chini ya miaka mitano ukiwemo unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita tangu mtoto anapozaliwa.

Mratibu wa Uhamasishaji na Uelimishaji Masuala ya Afya wa Mkoa wa Kagera, Nelson Rumbeli, alibainisha hayo katika hafla ya akinamama wenye watoto chini ya miezi sita iliyopewe jina la “Mother Meet Up” iliyofanyika jana katika Kata ya Kemondo, Bukoba.

Hafla hiyo iliyoandaliwa na serikali kwa ushirikiano na mradi wa USAID Tulonge Afya kupitia Jukwaa la Naweza, ilihusisha zaidi ya akinamama 50 wenye watoto chini ya miezi sita.

Alisema kushuka kwa kiwango hicho cha udumavu mkoani hapa kunatokana juhudi na msukumo wa serikali kuboresha huduma katika sekta ya afya.

Aidha, serikali imeendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo, ikiwemo USAID Tulonge Afya kuhamasisha malezi bora kwa watoto tangu wanapozaliwa hadi wanapofikisha umri wa miaka mitano.

Kwa mujibu wa Rumbeli, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo alizindua na kusaini mikataba na wakuu wa mikoa na ngazi mbalimbali za uongozi hadi ya vijiji ili kushughulikia lishe, jambo ambalo ni changamoto kwa maeneo mbalimbali nchini.

Alisema mwaka jana vifo vya akinamama wakati wa kujifungua mkoani Kagera vilikuwa 80 na mwaka huu vimepungua hadi 45 sasa.

Kupungua kwa vifo hivyo kumetokana na ongezeko la ujenzi wa hospitali, vituo vya afya na zahanati pamoja na ongezeko la dawa katika hospitali hizo.

Aidha, uhamasishaji na elimu waliyopata akinamama kuhusu umuhimu wa kuhudhuria kliniki wanapohisi kuwa na ujauzito, umetajwa kuwa sababu nyingine ya kupungua kwa vifo hivyo.

Mratibu wa Mradi wa USAID Tulonge Afya ngazi ya wilaya kutoka shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na masuala ya afya na mazingira (Tadepa), Benson Rweyemamu alisema lengo la “shughuli ya Mother Meetup” ni kutoa nafasi kwa akinamama wenye watoto chini ya miezi sita kujadiliana na kupeana uzoefu kuhusu malezi ya watoto tangu wanapozaliwa hadi wanapofikisha miaka mitano na kuwafanya wao kuwa mabalozi wazuri katika jamii zao.

Meneja Mradi wa Tulonge Afya kwa Kanda ya Ziwa, Sihiana Mkanda, alisema mradi wa miaka mitano unaotekelezwa kwa ufadhili wa shirika la Kimarekani la USAID katika mikoa 12 ya Tanzania.

Kwa Kanda ya Ziwa, mradi huo unatekelezwa katika wilaya 12 za mikoa ya Mwanza, Geita, Kagera, Mara, Shinyanga na Kigoma.

Mkoani Kagera mradi huo unatekelezwa katika wilaya za Muleba na Bukoba Vijijini.

Chanzo: habarileo.co.tz