Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uchunguzi wa kimaabara waanza maji ya mto Ngerengere

Povu Balaaaaa.jpeg Uchunguzi wa kimaabara waanza maji ya mto Ngerengere

Tue, 23 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mamlaka na taasisi nne za Serikali zimeanza uchunguzi wa kimaabara wa maji katika mto Ngerengere kutokana na kuchanganyika na povu linaloelezwa ni la kemikali, ambayo ni malighafi ya kutengeneza sabuni.

Mamlaka na taasisi hizo ni Bodi ya Maji Bonde la Wami-Ruvu, Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Maabara ya Maji na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (Nemc) Kanda ya Rufiji.

Mhandishi wa Mazingira wa Bodi ya Maji Bonde la Wami-Ruvu, Abdallah Mshana amesema wataalamu wameshachukua vipimo vya awali ili kuona kama kuna viashiria vya mabadiliko ya maji katika mto Ngerengere.

Akizungumza na Mwananchi Digital jana Januari 22, 2024 Mshana amesema timu ya wataalamu hao ilifika maeneo ya Nane Nane na Tungi ambako kulionekana povu jeupe kutoka kwenye korongo linalopitisha maji wakati wa mvua, ambayo yanatiririka kuelekea mtoni.

“Taarifa za wananchi zilienea kuwa mawingu yameshuka ardhini, lakini yale ni mapovu yaliyosababishwa na maji yaliyokuwa yakiporomoka kwa kasi na kuzalisha mapovu mengi. Timu yetu imeenda kuchukua sampuli na kupeleka maabara, tutapata majibu. Kwa sasa tumewazuia wananchi wasisogelee maeneo hayo wala kutumia maji mpaka vipimo vitakavyotoa majibu,” amesema Mhandisi Mshana.

Januari 21,2024 kulisambaa taarifa kwenye mitandao ya kijamii kukionekana video inayoonyesha povu jeupe, jamii ikiaminishwa kuwa ni mawingu yameanguka kutoka angani katika maeneo hayo.

Idara ya Afya Manispaa ya Morogoro, ilieleza hayakuwa mawingu bali povu lililotokana na msuguano wa maji uliochanganyika na kemikali ambayo ni malighafi ya kutengenezea sabuni.

Povu hilo linaelezwa lilikuwa na ukubwa wa kimo zaidi ya mita tano.

Kauli za wananchi

Baadhi ya wananchi wameieleza Mwananchi Digital kuwa kemikali ilimwagika baada ya madumu yenye malighafi hiyo kuanguka na kupasuka katika eneo la maegesho ya malori Nane Nane.

Amrani Kasongo, amesema Januari 16, 2024 saa nane mchana lori lililobeba shehena ya kemikali hiyo liliegeshwa ili kupakua mzigo na kuupanga upya kwenye kontena.

Amesema takribani madumu 10 yalikuwa yamepasuka na kemilikali kumwagika ardhini. “Dereva baada ya kuegesha gari ndani ya maegesho ya Nane Nane aliwataka vijana wapakue madumu na kuyapanga upya, lakini zaidi ya madumu 10 yalipasuka na kemikali ilimwagika ardhini. Baada ya kupangwa upya gari liliendelea na safari saa 12 jioni,” amesema Kasongo.

Amesema siku mbili baadaye, mvua kubwa ilinyesha na kusomba tope lenye kemikali kuelekea kwenye mifereji kisha kuingia kwenye korongo linaloelekea Tungi.

Wakati mvua ikisomba tope, amesema kulitokea povu jingi lenye kimo cha zaidi ya mita tano ambalo lilipeperushwa na upepo.

“Mapovu yalianza kuonekana eneo letu hapahapa maegesho ya malori Nane Nane, nimeshangaa mapovu yale kutafsiriwa kuwa ni mawingu meupe yamedondoka kutoka juu, jambo ambalo si kweli kwa sababu hawajui chanzo cha yale mapovu,” amesema Kasongo.

Kwa upande wake, Godfrey Joseph amesema yeye ni miongoni mwa waliochukua kemikali hiyo na kuitumia kufua nguo zake.

“Ile kamikali ipo kama ujiuji hivi, niliwaona wenzangu wakichota wakaitumie kama sabani, na mimi nilichukua nikafua nguo lakini zile nguo ukiwa umevaa na ikapata unyevu basi mwili huwa unawasha. Wapo waliohusika kushusha yale madumu wamebabuka sehemu za miili yao,” amesema Godfrey.

Mkazi wa Manispaa ya Morogoro, Happness Shayo amesema, “Watu wanapoona jambo ambalo ni geni kwao ni vizuri kutoa taarifa kwa uongozi wa eneo husika, na si sahihi kusambaza taarifa kwa njia yoyote kwa umma kwa jambo ambalo huna ujuzi nalo kwani linaleta taharuki isiyo ya lazima.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live