Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uchimbaji mchanga vyanzo vya maji tishio Dar

14609 MCHANGA+PIC TanzaniaWeb

Thu, 30 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Licha ya Serikali kupitia Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (Nemc) na Mamlaka ya Bonde la Ruvu kupiga vita uharibifu wa mazingira kwenye vyanzo vya maji, uchimbaji wa mchanga katika mito inayopita jijini Dar es Salaam umekithiri, huku mamlaka na wananchi wakirushiana lawama.

Wachimbaji wengi ni vijana wa kiume wakiuza kwa watu binafsi kwa ajili ya ujenzi. Uchunguzi wa Mwananchi katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam umeonyesha mchanga unaobebwa na malori ya tani saba ni kati ya Sh40,000 hadi 60,000 huku malori yenye uzito zaidi ya tani 10 ni Sh100,000 eneo la uchimbaji na likifikishwa kwenye eneo husika bei inaweza kufika hadi hadi Sh250,000.

Katika kata ya Kawe ambako Mto Mbezi unapita uchimbaji mchanga umesababisha mto huo kupoteza mwelekeo na kufurika, wananchi walikubaliana kuweka wakandarasi kuurekebisha mto huo mwaka jana. Hata hivyo, wananchi hao wameshikwa na butwaa kwa wakandarasi hao kugeuza operesheni hiyo kuwa mradi wa kuuza mchanga.

Diwani wa kata ya Kawe, Mutta Rwakatare anasema suala la usafishaji mto huo lilikubaliwa na wananchi wenyewe baada ya kutokea mafuriko.

“Suala si kuchimba mchanga, huu ni mto, wameomba wananchi wenyewe kufanyiwa usafi wa mto na mazingira yao, kutokana na mafuriko yaliyotokea mwaka jana Oktoba nyumba zaidi ya 550 zilipotea na 357 ziko katika hali mbaya,” anasema.

Aliongeza: “Bahati mbaya mto Mbezi ni mapokeo ya maji kutoka mikoani huko ili yaje kuingia baharini. Kwa hiyo ni lazima ufanyike usafi.”

Alisema hii si kwa wananchi pekee, imeshirikisha viongozi wa Nemc, Manispaa ya Kinondoni, Mamlaka ya Bonde la Ruvu na Wami na Ofisi ya mkuu wa mkoa.

Wakizungumza hivi karibuni katika mkutano ulioshirikisha wakazi wa kata ya Kawe, Nemc na Mamlaka ya Bonde la Ruvu, wananchi wameonyesha kukerwa na biashara hiyo ambayo wanadai inafanywa huku kinachoitwa kuusafisha mto kikiendelea.

“Nia ya Serikali kuleta tingatinga ni kusafisha mto, kwa hiyo uchimbaji mchanga sasa basi na mchanga uliorundikwa katikati uondolewe,” anasema May Maumba ambaye ni mkazi wa mtaa wa Mzimuni.

Malalamiko hayo pia alikuwa nayo Godfrey Mwaluko akisema wakandarasi hao hutumia muda mwingi kuchimba mchanga na kuuza kuliko kutekeleza kazi ya kusafisha mto.

“Tulikubaliana wasafishe mto kisha wapande matete, lakini kinachofanyika ni kuchimba mchanga. Oktoba haiko mbali mvua itaanza tena,” alisema Mwaluko.

Maoni hayo yameungwa mkono na Kusiriwa Mwasha akisema: “Hata kama hao wakandarasi wana vibali wangekuwa wanarekebisha kingo za mto kwanza, badala yake wamesababisha mto uongezeke, wakati zamani ulikuwa mbali.”

Hata hivyo, Steven Kayuni aliyewahi kuwa mkandarasi katika eneo hilo ametetea uchimbaji wa mchanga akisema unasaidia wakandarasi hao kufidia gharama za operesheni hiyo.

“Mkandarasi lazima aruhusiwe kuchimba kwa sababu zile mashine zinakodishwa na zinalipiwa mchana na usiku, asipouza mchanga atapata wapi fedha za kujazia gharama hizo,” anasema Kayuni.

Mkandarasi wa kampuni ya Othyblue International, Heri Mohammed aliyekuwepo katika mkutano huo amesema malalamiko ya wananchi hao yana sura ya kisiasa na kiuchumi.

“Wengi wanaopinga kazi hii ni wanachama wa Chadema na wanaounga mkono ni CCM. Halafu kuna watu walikosa tenda ya kazi hii, ndio wanahamasisha wananchi kupinga kazi yetu,” anasema Mohammed.`

Mwakilishi wa Mamlaka ya Bonde la Wami Ruvu, Mshube Wilson aliwataka wananchi hao kupeleka malalamiko yao kwenye kamati ya mazingira ya kata badala ya kuwasumbua wakandarasi wawapo kazini.

Nemc washtuka

Akizungumza katika mkutano huo, Mwanasheria wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (Nemc), Heche Suguta amewaonya wakandarasi hao akiwataka wafanye kazi kulingana na mikataba yao.

“Wengi mmesema kazi iendelee ila kuwe na usimamizi mzuri. Hizi kazi zinafanyika kwa nyaraka, tutaangalia mpango kazi wao. Je, wanafuata sheria? Mbona wanachimba mchanga tu?” Alihoji Heche.

Akizungumza na Mwananchi baada ya mkutano huo, Heche alisema tathmini nzima inaonyesha kinachoendelea kwenye mto huo ni biashara ya mchanga hivyo Nemc haikusudii kuwaruhusu wakandarasi hao kuendelea na kazi.

Polisi wahusishwa

Mbali na Kawe, biashara ya mchanga imeonekana kukithiri katika maneo ya Makongo Juu na Goba unakopita mto Mbezi, huku Jeshi la Polisi lihusishwa.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Makongo Juu, Obadi Mbelwa ameliambia Mwananchi kwa njia ya simu kuwa tatizo la uchimbaji wa mchanga katika bonde la mto Mbezi limekuwa sugu licha ya wananchi kulalamika kwa muda mrefu, huku akilihusisha Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni.

“Hilo ni tatizo sugu tumeshawahusisha polisi na wahalifu walishapelekwa Polisi Oysterbay, lakini hakuna tunachoona, badala yake wanaendelea tu kuchimba,’ alisema na kuongeza:

“Mimi nilipoingia madarakani mara ya kwanza (2014), niliwashirikisha wananchi wa maeneo ya pale kufanya ulinzi shirikishi. Nilifanya operesheni lakini nilichoambuliwa ni kutaka kupigwa. Polisi wanapokuja maeneo yale wanamalizana na wachimbaji.”

Ameelekeza pia lawama zake kwa wakazi wa maeneo hayo akisema baadhi nyumba zao hazijakamilika hivyo nao hushiriki kuchimba mchanga wa kujengea, huku wakishindwa kufanya ulinzi shirikishi.

“Dawa ni hao hao wananchi, kwa nini mchanga uchimbwe na wao wapo?” Alihoji.

Licha ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Jumanne Muliro kusema ameipokea taarifa hiyo na anaifanyia uchunguzi, alisema jeshi hilo lisihusishwe na kila kitu.

“Hii nchi inaendeshwa kwa utawala wa sheria na kuna vyombo vya kisheria vinavyosimamia mambo. Suala hilo zipo mamlaka za mazingira,” alisema na kuongeza:

“Yaani mi niache kukamata wahalifu wangu, nikalie kukimbizana na mambo yenye vyombo vyake vinavyosimamia? Nimepokea hiyo taarifa tutafanya uchunguzi.”

Hata hivyo, mwenyekiti wa mtaa wa Kibululu, kata ya Goba, Steven Lipangile amesema wamekuwa wakishirikiana na Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi kupambana na wachimba mchanga.

“Hilo suala tumelishughulikia kwa muda mrefu ikiwa pamoja na kuvishirikisha vyombo vya ulinzi na usalama likiwemo Jeshi la Wananchi kwa sababu tunapakana na kambi ya Changanyikeni,” anasema na kuongeza:

“Hapo kuna gari la polisi huwa linazunguka kwenye machimbo hapo na risasi zinatumika na maofisa wa Nemc pia wanakuja. Tulikuwa na kikao cha wananchi na polisi walihusika na kukubaliana kuweka vizuizi ili malori yasiende kwenye machimbo.”

Katika eneo la Makongo Juu, mmoja wa wachimbaji aliyejitambulisha kwa jina moja la Fadhili alisema rundo moja la mchanga linauzwa kati ya Sh25,000 hadi 30,000.

“Mchanga unauzwa Sh30,000 lakini lori unajilipia mwenyewe. Si rahisi kukamatwa kwa sababu hapa kuna wachimbaji, kuna waangalizi,” alisema mchimbaji huyo.

Alitaja maeneo yanayopatikana mchanga kwa wingi kuwa ni karibu na shule ya sekondari ya St Columbus, karibu na kanisa katoliki na karibu na Kambi ya Jeshi ya Lugalo ambako hata hivyo alisema ulinzi umeimarishwa.

Chanzo: mwananchi.co.tz