Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uchafuzi wa mazingira wawakutanisha wadau Dar

Thu, 28 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wadau wa mazingira kutoka taasisi mbalimbali wamekutana kwa siku moja jijini Dar es Salaam kujadili awamu ya mwisho ya mpango wa taifa wa kuzuia uchafuzi wa mazingira.

Mkutano huo unaoratibiwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) na kuwezeshwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (Unido), lengo lake ni kukamilisha mpango huo utakaotekelezwa kwa awamu tano.

Akizungumza kwenye mkutano huo leo Alhamisi Februari 28, 2019  Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Afya na Usafi wa Mazingira kutoka Wizara ya Afya, Theophil Kangaga amesema uchafuzi wa mazingira ni chanzo cha maradhi mbalimbali, vifo na hata ulemavu, hivyo Wizara ya Afya na Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira ziliandaa andiko ambalo kimsingi ni mpango mkakati wa taifa wa kukabiliana na hali hiyo.

"Tunalipitia kwa mara ya mwisho kabla ya kulipeleka kwa wadau kwa ajili ya kuliombea fedha kwa wafadhili," amesema Kangaga.

Amesema mradi huo utakuwa na awamu tano, kila moja itagharimu Euro milioni 5 ambapo kwa ujumla hadi kukamilika utagharimu Euro 25 milioni ambazo hazipungui  Sh66 bilioni.

Amefafanua mpango huo utalenga maeneo matano yakiwamo kuzuia uchafuzi wa mazingira utokanao na hali ya hewa wa nje ya nyumba na ndani ya nyumba, kuzuia uchafuzi wa maji, kuzuia uchafuzi wa mazingira utokanao na matumizi ya viutilifu.

Kwa upande wake mwakilishi wa Unido nchini Tanzania, Dk Stephen Kargbo amesema  kwenye mpango huo watawalenga wakulima, wachimbaji wadogo na wananchi.

"Uchafuzi wa hali ya hewa upo karibu kila mahali majumbani, nje ya nyumba, kwenye maji, hivyo tutashirikisha jamii nzima" amesema Dk Kargbo.

Jarida la Lancet katika utafiti wake mwaka 2015 ulionyesha uchafuzi wa hewa huua watu 6.5 milioni kila mwaka ikifuatiwa na uchafuzi wa maji, ambao huua watu milioni 1.8. Utafiti huo ulionyesha asilimia 92 ya vifo vilivyotokana na  uchafuzi hewa vilitokea kwenye nchi zinazoendelea.



Chanzo: mwananchi.co.tz