Dar es Salaam. Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo imezindua wiki ya mazingira mwaka huu yenye kauli mbiu ya kupinga matumizi ya mifuko ya Plastiki ambayo kuanzia kesho hairuhusiwi kutumika wala kuzalishwa nchini.
Uzinduzi huo umefanyika leo Mei 31, 2019 katika viwanja vya Manzese Bakhresa, ambapo mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi wa halmashauri na viongozi wengine katika manispaa hiyo walihudhuria.
Katika hafla hiyo Mkuu Wilaya Kisare Makori amesema suala la marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki lina nguvu ya kisheria lakini linahitaji uhamasishaji kwa wananchi na kuwaeleza madhara ya mifuko hiyo na faida za kuacha kuitumia sanjari na kuwaeleza njia mbadala.
"Mifuko hii ya plastiki haiozi na kuwa mbolea kama taka nyingine lakini pia inaziba mitaro na mifereji ya maji machafu na kusababisha magonjwa ya milipuko hivyo marufuku hivyo inalenga kutunza mazingira," amesema Mkori akiongeza na wananchi waliofika katika viwanja hivyo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo Beatrice Dominic amesema tayari ofisi yake imezungumza na mkandarasi anayekusanya taka katika halmashauri hiyo na kukubaliana kutenganisha taka za mifuko ya plastiki na nyinginezo zinazoweza kuoza lakini pia kuwa vituo zaidi ya 14, vimeandaliwa kukusanya mifuko hivyo inayosalimishwa na watu.
"Natoa wito kwa watu kusalimisha mifuko yako katika vituo vilivyopo kila kata, watu wasichanganye mifuko hiyo na taka nyingine ... tutakuwa na zoezi la kutoa elimu kwa siku 30 kuanzia kesho ili watu kuelewa utaratibu na kufuata marufuku hii," amesema Dominic.