Mbunge wa jimbo la Ulanga Mkoani Morogoro, Alaudin Hasham amesema amesikitishwa na ucheleweshwaji wa ukarabati wa barabara ya Lupiro hadi Ulanga na kitendo cha TANROAD kupeleka mkandarasi asiyekuwa na vifaa.
Akizungumza na Wanahabari Mkoani huko, Hasham amesema barabara hiyo imeharibika kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha na imesababisha athari za maafuriko pamoja na uaribifu wa miundombinu kwa takriban miezi minne sasa.
Amesema, “mbaya zaidi ambacho kimeniuma kutoka kwa TANROADS ni kwamba anapigiwa simu mkuu wa TANROADS mkoa anasema alishapata mkandarasi lakini mkandarasi hana vifaa ni akili za kawaida kweli unampa mkandarasi hana vifaa ndo aje atuhudumie sisi.”
Akijibu madai hayo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro, Kymba Alinanuswe amesema barabara zote za Morogoro zina mkandarasi na tayari anafanya kazi lakini si jukumu lake kujua mkandarasi anapata wapi vifaa badala yake anataka kazi ifanyike.
Mvua hizo, zimeathiri maeneo mbalimbali Nchini na kusababisha vifo pamoja na uharibifu wa makazi, mashamba na miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara.