Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

UVUMI: Ebola feki yaleta taharuki Moshi

60654 Poc+ebola

Fri, 31 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Taharuki ilitanda katika Mji wa Moshi jana baada ya kuenea kwa taarifa za uwapo wa mgonjwa wa Ebola Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Kilimanjaro, Mawenzi.

Taarifa za kuwapo kwa mgonjwa hospitalini hapo, zilianza kuenea saa 3:00 asubuhi baada ya kudaiwa amebainika kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) akitokea nchini DRC Congo.

Baada ya kuenea taarifa hizo wananchi kwa makundi walijaa barabarani huku wakielekea karibu na jengo maalumu la magonjwa ya mlipuko hospitali hapo ambako walikaa nje.

Taharuki ilizidi baada ya kuonekana gari la kubeba wagonjwa likiingia hospitalini huku watu waliokuwa wamevalia vifaa vya kujikinga na magonjwa ya mlipuko wakishusha mtu aliyedaiwa mgonjwa wa Ebola.

Licha ya kuonekana mtu aliyedaiwa mgonjwa akishushwa, wananchi wengi walionekana kutokuwa na uelewa wa ugonjwa huo kama ni hatari, walitaka kusogelea gari hilo ili kumuona.

Akizungumzia tukio hilo, mganga mkuu mkoa wa Kilimanjaro, Dk Best Magoma alisema hakuna mgonjwa wa Ebola bali walitaka kujua utayari wa watumishi wa hospitali hiyo na idara nyingine wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

Pia Soma

“Hakuna mgonjwa wa Ebola Kilimanjaro, kikubwa tulikuwa na zoezi jumuishi kati ya sekta ya afya na wenzetu wa Kia, lengo likiwa ni kuangalia namna tulivyojiandaa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko,” alisema.

Naye kaimu ofisa afya mkoa wa Kilimanjaro, Uforo Mariki alisema wana kazi kubwa ya kuelimisha wananchi kuchukua tahadhari iwapo kutatokea magonjwa ya mlipuko, kwani wengi hawajui kuwa ni hatari.

Chanzo: mwananchi.co.tz