Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

UTHUBUTU: Kutoka kuuza matikitiki hadi kuendesha tingatinga

81049 Pic+matikiti UTHUBUTU: Kutoka kuuza matikitiki hadi kuendesha tingatinga

Mon, 21 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Ukiwa kwenye viunga vya mji wa Dodoma ni jambo la kawaida kukutana na greda la halmashauri ya manispaa ya mji huo likiendeshwa na mwanamke.

Mwanamke huyo ni Easter Nyinge (27) pamoja na kuwa na mwili mdogo lakini anaendesha greda hilo na kuwa kivutio kwa baadhi ya wakazi wa mji huo.

Wengi wana imani kuwa greda au tingatinga kama linavyoitwa na wengi, huendeshwa na wanaume ndiyo sababu hasa ya kuwafanya wengi kushangaa.

Easter aliishia kidato cha pili na huenda ndio sababu ya kupata ujasiri wa kufanya kazi yoyote ikiwam kuendesha greda.

Hakufika hapo kama ndoto, amepambana na amejaribu kazi nyingi ikiwamo kuuza maitikiti maji mitaani.

“Ujasiri, kuthubutu ndiyo kumenifikisha hapa nilipo”anasema.

Pia Soma

Advertisement
Easter anasema mwaka 2009 akiwa tayari amemaliza elimu ya msingi na kuanza sekondari, baba yake aliyekuwa mtimishi wa Serikali alifariki dunia akimuacha na mama yake aliyekuwa kibarua katika kampuni za ujenzi wa barabara.

Baada ya kumaliza darasa la saba hakuchaguliwa kujiunga na masomo ya sekondari hivyo alijiunga na shule ya kulipia lakini kutokana na ukosefu wa ada aliishia kidato cha pili. “Mama alikosa fedha za ada ilinilazimu kukatisha masomo mwaka 2013 nikiwa kidato cha pili,’’ anasema bila kutaja jina la shule.

“Niliamua kufanya kazi ya ujenzi wa barabara kama kibarua katika kampuni ya GNMS Mungai,” anasema. Akiwa na GNMS alikuwa akifanya kazi ndogo ndogo kama kuwasha pampu za maji na kuweka maji katika maboza.

Baada ya kufanya kazi miaka mwili na nusu aliamua kujiendeleza. “Niliona sina elimu na kazi nilizokuwa nikifanya ni ngumu lakini pia malipo ni madogo. Nilikuwa nikilipwa Sh5,000 kwa siku,” anasema.

Aondoka Iringa

Mwaka 2015 aliondoka Iringa na kwenda Kondoa ambako kulikuwa na kampuni ya ujenzi wa barabara ya Chico iliyokuwa ikijenga barabara kwa kiwango cha lami na kupata kazi ya kibarua kwenye kampuni hiyo na alikuwa akilipwa Sh12,500.

“Nilifanya kazi kama utingo wa gari zilizokuwa kwenye mradi, lakini nilikuwa bado nina wazo la kujiendeleza hivyo kila nilichofanya sikuwa mbali na wazo la kujiendeleza,” anasema.

Anafafanua kuwa mwaka 2016 mradi ulimalizika na akarudi nyumbani Iringa.

“Niliporudi nilikwenda kujiunga na dada mmoja aliyekuwa akijishughulisha na upambaji katika sherehe mbalimbali, alikuwa akinilipa Sh20,000 kila nikifanya kazi, ambazo zilinisaidia kununua chakula,” anasema.

Baada ya hapo alijiunga na watu wa kusajili namba za simu za Vodacom na alikuwa akipata Sh1,000 kwa kila laini aliyoiuza kipato ambacho anasema kilikuwa kidogo, hivyo akafikiria ni mji gani anaweza kuishi na kupata angalau kibarua chenye nafuu.

“Baadaye niliona kuwa Dodoma kwa sababu ni karibu na nyumbani, nikipata tatizo naweza kurudi.

Anasimulia kuwa alifikia nyumba ya wageni alikoishi siku saba na kuwaomba wahudumu kama wanafahamu mahali anakoweza kupata chumba cha kupanga cha gharama nafuu.

Anasema alipata chumba eneo la Makole kwa Sh10,000 kila mwezi. “Niliamua kuanza biashara ya kuuza matikiti. Niliyanunua Soko la Sabasaba kwa mtaji wa Sh17,000 nakatakata naweka katika deli na kuuza Sh 200 kila kipande,” anasema.

Mtaji wa kununulia matunda na chombo cha kuhifadhia, aliupata baada ya kuiweka rehani dukani simu yake yenye thamani ya Sh20,000.

Ili kumudu maisha kuna wakati alikuwa hauzi matunda bali alifanya vibarua vya ujenzi ambapo alikuwa akipata fedha ya chakula.

Akiwa katika kuuza matunda, alikutana na mtumishi wa manispaa na kumweleza kuwa anatamani kuendesha greda au mitambo ya ujenzi.

Mtumishi yule alichukua namba yake ya simu na baada ya wiki moja alimpigia akitaka waonane. Alikwenda kuanza kuzunguka naye kwenye shughuli za manispaa akijifunza vitu mbalimbali.

Alivyoelewa baadhi ya vitu alijaribu bahati kwa kuomba kazi kwenye halmashauri hiyo, badala ya kufanya juu juu. “Nilionana na ofisa usafirishaji ambaye alinipeleka idara ya mazingira.

“Nikapelekwa kwa ofisa utumishi ambaye aliagiza nifanyiwe mahojiano na nikiweza nipewe kazi. Baada ya mahojiano niliondoka, baada ya siku kadhaa nilipigiwa simu kujulishwa nimepata kazi,” anasema.

Aliajiriwa kama dereva wa greda la halmashauri linalofanya kazi mbalimbali ikiwamo kubomoa nyumba inapohitajika.

Anasema kazi hiyo angalau ilimsaidia ikiwamo kumlipia ada mtoto wake Shule ya City Maria.

“Kuna watu hadi leo wanashindwa kuamini kuwa naendesha greda hili kwa sababu mimi mwanamke, wanaamini wanaume ndiyo wanastahili kuliendesha. Kuna wakati wananitolea maneno makali hasa ninapokwenda katika masoko kukusanya taka,” anasema.

Anasema amekuwa akisafisha mji kwa manufaa yao lakini wanaona kama wanaonewa. “Na wanaonifanyia hivi ni wanawake wenzangu wanashindwa kunipa ushirikiano, wanashindwa kuelewa hata watoto wao wanaweza kuja kuifanya kazi hii, wananitenga, wananichukia,” anasema.

Anasema kazi hiyo inahitaji ujasiri hasa wanapofanya kazi ya kubomoa nyumba za watu ambazo hazikufuata masharti ya ujenzi. “Wasio waelewa wananichukia na kuniwekea fitina. Wanasema wamejenga nyumba zao kwa jasho na mimi nakuja kuwabomolea,” anasema huku akihuzunika.

Anasema anatamani wajue kuwa ni sehemu ya kazi na wajifunze wakati mwingine kuwa makini wanapotaka kuwekeza hasa kwenye ujenzi wajiridhishe kama eneo husika ni salama.

“Nikitumwa natekeleza, nakutana na mengi ila Mungu amekuwa akinipigania,” anasema.

Anasema hatosahau pale walipoenda katika ubomoaji eneo la Chang’ombe Kisima cha Nyoka ambapo walikutana na nyuki waliokuwa ndani ya nyumba hali hiyo iliyowafanya kuliruka eneo hilo na kuendelea eneo jingine.

Ushauri watoto wa kike

Anawashauri watoto wa kike kusoma kwa bidii na wazazi kuwalea watoto katika maadili mazuri na misingi ya kidini.

“Natamani wazazi waandae maisha ya watoto kwa miaka 10 ijayo, ili ikitokea wamefariki au kupata majanga ya maisha wawe na uhakika wa kupata elimu.

“Leo pamoja na ugumu wa maisha, bado nina deni la kujiendeleza kielimu, lakini ningesoma wazazi wangu wangekuwa na uwezo au mipango ya jinsi nitakavyosoma baadaye,” anasema.

Anawaasa wasichana, wanawake kutoangalia walikoanguka, badala yake kusonga mbele kwa sababu kutazama nyuma ni kushindwa.

Chanzo: mwananchi.co.tz