Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

UCSAF yaangalia uboreshaji usikivu wa TBC, RFA

Fd361fdc2cc4542bc2db968fb7bb9210.jpeg UCSAF yaangalia uboreshaji usikivu wa TBC, RFA

Fri, 7 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MFUKO wa Mawasiliano Kwa Wote (UCSAF) unafanya mazungumzo na Shirika la Utangazaji (TBC) na Radio Free Africa (RFA) kuona namna ya kuboresha urushaji wa matangazo katika maeneo ya pembezoni ambayo ni maskini kiuchumi.

Ofisa Mtendaji mkuu wa UCSAF, Justina Mashimba alisema taasisi yake inafanya mazungumzo na TBC namna ya kuboresha usikivu katika maeneo ya mipakani ikiwamo Kagera, Kyela, Ruvuma, Njombe, Ludewa na Katavi.

“Pia tunashirikiana na RFA kuimarisha usikivu katika wilaya za Mlele, Gairo, Kondoa na Tanganyika,”alisema Mashimba na kuongeza kuwa ingawa maeneo hayo yana vifaa vya kisasa vya mawasiliano hasa simu, usikivu wa matangazo ya radio ni mbaya katika baadhi ya maeneo.

Mtendaji huyo alisema kwamba uboreshaji wa huduma za mawasiliano katika maeneo hayo ya pembezoni yatasaidia kuimarisha maendeleo na demokrasia vitu ambavyo ni msingi wa kuanzisha kwa mfuko huo.

UCSAF ilianzishwa mwaka 2006 kuhakikisha kwamba maeneo ya pembezoni yanapata huduma za mawasiliano kwa gharama nafuu kunakuwapo na huduma za mawasiliano kwa bei nafuu. Wakati wa kuanzishwa kwa taasisi hiyo asilimia 80 ya wakazi wa Tanzania walikuwa wanaishi vijijini wakikabiliwa na changamoto ya mawasiliano.

Huduma za mawasiliano zinazozungumzwa ni pamoja na posta, radio na televisheni.

Meneja wa fedha na utawala wa UCSAF, Pius Joseph alisema taasisi hiyo imetoa zaidi ya Sh bilioni 150 kusaidia miradi mbalimbali ya mawasiliano nchini.

Alisema kwa sasa taasisi hiyo imekuwa ikitoa ruzuku kusaidia stesheni za radio kupata umeme wa njia tatu ili kusaidia urushaji wao wa matangazo.

Wakati huo huo, Meneja wa Operesheni wa taasisi hiyo Idd Mlua alisema zaidi ya kata 700 zimefikiwa na ruzuku zinazotolewa huku na sasa wanafikiria kuiunganisha hospitali ya Benjamin Mkapa ya Dodoma na Mnazi Mmoja iliyopo Unguja ili kuweza kuwa na huduma tiba za mtandao (telemedicine).

Mchakato huo unatarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha wa 2020/21 na utahusisha ujenzi wa vituo 10 vya Tehama Tanzania Bara.

Chanzo: habarileo.co.tz