Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tuyuli; jamii ya kaa ‘mwizi’ wa nazi

6993f6124127aecf150168ef5bb63746.png Kaa aina ya Tuyuli

Fri, 17 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MAONESHO ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) yaliyomalizika Julai 13, mwaka huu, yalifanyika kwa mafanikio makubwa ingawa sio kama miaka mingine.

Hali hiyo ilitokana na dunia kukumbwa na mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) ambapo nchi mbalimbali duniani zimeathirika na tatizo hilo, ikiwemo Tanzania.

Athari za corona katika nchi duniani ni pamoja na kusitishwa kwa safari za ndege za kimataifa, na uchumi kushuka kwa kiwango fulani katika nchi hizo huku athari zake zikionekana zaidi kwenye nchi zilizoathirika kwa kiwango kikubwa.

Pamoja na yote, bado shughuli mbalimbali za uchumi nchini ziliendelea baada ya hali kutengamaa mwishoni mwa Mei mwaka huu kwa mataifa mengi ambayo yalifungua rasmi masuala ya uchumi na kazi kuendelea huku Tanzania nayo ikiwataka wananchi wake kuendelea kuchapa kazi kwa kuchukua tahadhari.

Ni katika muktadha huo, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara nchini (TanTrade) iliratibu maonesho hayo ya biashara ya kimataifa ambayo kwa mwaka huu jumla ya washiriki 2,880 wa ndani na nje walipata fursa ya kuonesha bidhaa na huduma wanazotoa.

Katika mambo yaliyovutia washiriki wa maonesho hayo, ni pamoja na ubunifu wa vitu na bidhaa mbalimbali za ndani sambamba na teknolojia mpya na rahisi zilizotumika kuleta ubunifu wa vifaa vyenye tija kwa jamii kama vile vifaa tiba, sabuni na mashine mbalimbali.

Katika maonesho hayo, moja ya kivutio kikubwa kilikuwa ni kaa aitwaye tuyuli, ambaye ni jamii ya kaa lakini mwenye sifa ya kutokujua kuogelea na pia hujulikana kama kaa mwizi kutokana na tabia yake ya kuiba nazi mtini au ugali kwa wanavijiji.

Akimzungumzia kaa huyo katika banda la Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU), Mhifadhi Utalii, Davis Mpotwa anasema kaa huyo ni moja ya viumbe wa baharini walio kwenye hatari ya kutoweka kutokana na wavuvi na watu kuwaua ili kupata kitoweo na wengine kuona ni viumbe waharibifu.

“Tuyuli tumemleta Sabasaba kwa mara ya kwanza na amekuwa kivutio kwa wananchi wanaotembelea maonesho haya, kwanza ni jamii ya kaa asiyejua kuogelea na anaishi kwenye mapango maeneo ya pwani, chakula chake ni nazi, na vitu vingine lakini pia akikuta chakula au ugali anaiba, anakula,” anasema Mpotwa.

Anasema tuyuli ni jamii ya kaa mwenye ana uwezo wa kuwa mrefu hadi futi tatu na uzito wa kilogramu nne hadi tano na anaishi miaka 60 lakini pia anataga mayai zaidi ya 500, yanayoanguliwa ni machache kutokana na tabia yake ya kutotulia hivyo kufanya samaki kuyala na mengine kuharibika.

Tuyuli ana tabia za ajabu; kwanza hutaga mayai yake kwenye miamba pembezoni mwa bahari na bara baada ya mayai kuanguliwa watoto wake huvaa magamba ya konokono kwa ajili ya kujilinda kwa sababu ngozi zao ni laini na wakianza kuwa wakubwa hujivua gamba na kuendelea na maisha yao kwani huwa na uwezo wa kujilinda wenyewe.

Mpotwa anasema tuyuli hajui kuogelea, tofauti na kaa wengine na kwamba huishi zaidi maeneo ya Pwani kwenye mapango na hupenda zaidi kutembea na kula usiku kwa kupanda minazi kula nazi hivyo wananchi wa Pwani huwaua zaidi kwa kuwa wanasema ni waharibifu.

“Hawa tuyuli ni viumbe walio hatarini kupotea, wanapatikana maeneo machache sana duniani ikiwemo Tanzania na hata hapa nchini wanaonekana zaidi kwenye Kisiwa cha Mbudya, Dar es Salaam ambacho bado kiko salama, hakijaharibiwa,” anaeleza Mpotwa.

Tuyuli hana uwezo wa kukaa majini kwa muda mrefu, na akiingia majini hukaa sio zaidi ya saa moja kisha hutoka na kwenda nchi kavu kwenye mapango kutafuta malisho ikiwemo kupanda kwenye miti ya minazi kula nazi.

Kaa huyo ukimuona sio mkubwa sana, ni wa wastani lakini tabia zake ndizo zinaacha vinywa wazi wananchi hususan wa Pwani. Moja ya tabia yake ambayo wenyeji wa maeneo hayo wanaitaja kuwa ni mbaya ni tabia ya udokozi wa chakula.

“Wakazi wa Pwani wanawaua sana tuyuli kwa sababu wakiacha chakula nje kaa huenda kufunua na kuiba, pia hupanda minazi na kwenda kula nazi sasa wakazi hao wanawaua sana ili wasiharibu mazao yao,” anasema Mpotwa na kuongeza kwamba anapatikana pia kisiwani Chumbe, Zanzibar.

Nchi mbalimbali duniani zimepiga marufuku ya kumuuza au kumsafirisha kaa huyo kwa kuwa ni kiumbe adimu aliye hatarini kutoweka. Mfano nchini, Ufilipino, ni marufuku kumuuza kaa huyo, kadhalika kwa mujibu wa Mkataba wa Kimataifa wa biashara ya viumbe adimu vilivyo hatarini kutoweka (CITES), nao umekataza kufanya biashara ya viumbe hao.

Kaa hao katika baadhi ya jamii duniani huwatumia kama kitoweo, lakini kwa kuwa ni viumbe adimu duniani, sheria mbalimbali zimepiga marufuku uvunaji wake, lakini bado baadhi ya migahawa na hoteli zinauza kaa na wako kwenye menu zao za chakula.

Mpotwa anasema, juhudi za MPRU ni kuhakikisha viumbe hao adimu wanaendelea kuwepo kwa sababu hivi sasa hawaonekani maeneo mengi kutokana na wao kuogopa vurugu na ndio maana wamekimbilia kisiwa cha Mbudya ambacho bado hakijaharibiwa na shughuli za wananchi au wavuvi.

Katika kisiwa hicho kivutio kimojawapo cha watalii ni kwenda kuwaona tuyuli. Ni kaa wakubwa ambao wanashangaza kwa jinsi walivyo na zaidi ni hizo tabia zao za kuiba nazi mtini na wakati mwingine kuiba chakula kama ugali wakati umehifadhiwa ndani au nje kwenye nyumba za wakazi wa Pwani.

“Tuyuli ni kivutio cha watalii. Nawashauri wananchi wafanye utalii wa ndani kwa kutembelea kisiwa cha Mbudya kujionea hawa kaa,” anasema Mpotwa

Chanzo: habarileo.co.tz