Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tushikamane Pamoja Foundation yaiomba Serikali isajili kituo chake cha kulewa wazee

21176 TAASISI+PIC TanzaniaWeb

Mon, 8 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es salaam. Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Tushikamane Pamoja Foundation inayojihusisha na kuhudumia wazee imeiomba Serikali kukamilisha mchakato wa usajili wa kituo hicho ili kiweze kuanza kutoa huduma.

Akizungumza leo Oktoba 6, 2018 kwenye maadhimisho ya Siku ya Wazee Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Rose Mwapachu amesema wameanza mchakato wa usajili tangu Desemba mwaka 2O17 lakini hadi leo mchakato huo haujakamilika.

Kituo hicho kilichogharimu zaidi ya Sh 5OO milioni kitahudumia zaidi ya wazee 5O ambao hawana ndugu na sehemu za kuishi.

"Tunaiomba Serikali kutukamilishia mchakato wa usajili kwa kuwa maombi yetu tulishayawasilisha ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo ili kuyapeleka Wizara ya afya toka Desemba mwaka jana," amesema Mwapachu.

"Kama mnavyoona kituo hiki kimeshakamilika tunasubiri tu kibali cha wizara ili kuanza kukaa kwa wazee hawa ambao kwa sasa wanakaa nyumba za kupanga," amesema.

Ameongeza katika kituo hicho ambacho kimeshakamilika ziko baadhi ya changamoto ikiwamo kutokuwapo majisafi ya bomba na ukosefu wa pampu kwaajili ya maji ya kisima.

Kwa upande wa ofisa ustawi wa jamii Manispa ya Ubungo, Zainabu Masilamba amesema kituo hicho kitakapokamilisha taratibu zote zikiwamo kupata usajili kitatoa huduma mbalimbali kwa wazee ili kupunguza changamoto kwa wazee wasiokuwa na makazi.

"Tunajua kuanzishwa kwa kituo hiki kitasaidia wazee wengi lakini kitakapokamilika taratibu za usajili yako mambo mengi yatakayofanyika ili kuwaondolea wazee hawa changamoto za kimaisha" amesema Zainabu.

Mmoja wa wazee waliohudhuria Rajabu Kondo (67) amesema kuanzishwa kwa kituo hicho kitawasaidi wazee wasiokuwa na makazi yakuishi wala ndugu kukaa kwa pamoja .

"Tunaona mazingira haya yalivyo yatawezesha wazee kukaa na kufanya shughuli zao kwa pamoja bila kwenda kuombaomba," amesema Mzee Kondo.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz