Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tunduru wazindua kampeni kutokomeza kifua kikuu

9ea23c971d07cd4e24336332756ab65c Tunduru wazindua kampeni kutokomeza kifua kikuu

Tue, 26 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

HOSPITALI ya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, imezindua rasmi kampeni ya kutokomeza maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu mwaka 2021.

Aidha kwa mara ya kwanza wanachama wa Chama cha Msalaba mwekundu watatumika kama mkakati wa kupunguza maambukizi na kuwaibua watu wengi wanaougua ugonjwa huo.

Wanachama hao wataungana na wataalamu wa kitengo cha kifua kikuu na ukoma wa hospitali ya wilaya katika kutokomeza ugonjwa huo ambapo kwa mkoa wa Ruvuma wilaya hiyo inaongoza kwa maambukizi makubwa ya kifua kikuu.

Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Tunduru, Dk Mkasange Kihongole amesema wameamua kuwashirikisha wanachama wa Chama cha Msalaba Mwekundu kutokana na umuhimu wao katika jamii.

Alisema uzinduzi huo utakwenda sambamba na kufanya kampeni ya kuelimisha na kuchunguza vimelea vya ugonjwa huo.

Dk Mkasange alisema wale watakaobainika kuwa na ugonjwa huo wataanzishiwa dawa zinazotolewa bure katika zahanati,vituo vya afya na hospitali zote na kuiomba jamii kushirikiana katika kampeni ya mwaka huu.

Kwa mujibu wa Dk Mkasange, kauli mbiu ya kampeni ya kifua kikuu mwaka 2021 ni kifua kikuu katika wilaya ya Tunduru ni ya watu wote kwa kila mmoja ana wajibu kutokomeza ugonjwa huo.

Akizindua kampeni hiyo, mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Agostino Maneno, amewapongeza wanachama wa Chama cha Msalaba Mwekundu kwa kukubali kuwa sehemu ya timu ya kampeni ya kutokomeza ugonjwa huo na kuwataka kwenda kushiriki kikamilifu katika kuwaibua wagonjwa wengi wa kifua kikuu.

Alisema, lengo la serikali siku zote ni kuboresha afya za wananchi wake na kuwataka watendaji wa vijiji,mitaa na kata kuwapa ushirikiano wanachama hao pale wanapofika katika maeneo yao kwa ajili ya kutekeleza kazi hiyo .

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Dk Wendy Robert alisema kuna mikakati mbalimbali ya kuibua wagonjwa mengi zaidi wa kifua kikuu.

Alisema mwaka huu nguvu kubwa itatumika katika kuibua wagonjwa wa kifua kikuu hasa baada ya kuona katika wilaya hiyo kuna wagonjwa.

Chanzo: habarileo.co.tz