Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tunduru wasaka wezi wa dawa za kupulizia mikorosho

625ea88ab71b27d8fdc4370679b33b25 Korosho

Fri, 17 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SERIKALI ya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma imeanza operesheni ya kuwakamata viongozi wa Vyama vya Ushirika vya Kilimo (Amcos) ambao wanajihusisha na wizi wa dawa za kupulizia mikorosho zilizotolewa kwa ajili ya kuwakopesha wakulima wa zao hilo.

Tayari Jeshi la Polisi wilayani humo linamshikilia mjumbe mmoja wa Chama cha Ushirika cha Mlingoti Magharibi, Hamidu Mohamed kwa tuhuma ya kuuza mifuko 40 ya dawa hizo aina ya Sulphur.

Mkuu wa wilaya hiyo, Julius Mtatiro alisema hayo jana wakati akizungumza kwenye kikao cha kazi na baadhi ya viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika kutoka maeneo mbalimbali mjini Tunduru.

Alisema operesheni hiyo inalenga kukomesha vitendo vya wizi na dhuluma vinavyofanywa na viongozi wa vyama vya ushirika ambao kama wataachwa na tabia hiyo kuna hatari kubwa ya wakulima kukosa pembejeo, hivyo kushuka kwa uzalishaji wa korosho.

Alisema mara kwa mara amekuwa akipokea simu za malalamiko kutoka kwa wanachama wa vyama hivyo wakilalamikia tabia ya viongozi wao kuzidisha bei ya sulphur, wengine kutozwa fedha na watendaji wa vijiji wanapokwenda kuhitaji kugonga muhuri barua za maombi ya sulphur.

Kwa mujibu wa Mtatiro, bei elekezi ya dawa ni Sh 32,000 kwa mfuko mmoja wa kilo 25, lakini kutokana na tamaa baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika wanauza dawa hizo kati ya Sh 33,000 hadi 35,000.

Mtatiro amevitaja baadhi ya vyama vya ushirika vinavyolalamikiwa na wanachama wake ni Namungo, Mtonya, Mtetesi, Namsosa, ambapo ametishia kuwachukulia hatua kwani wanafanya kazi kinyume cha sheria.

Aidha ametoa siku saba kwa viongozi wa vyama hivyo kuhakikisha wanarudisha fedha walizochukua kutoka kwa wakulima kwa kuzidisha bei ya sulphur na watendaji wote wa vijiji waliotoza fedha za mihuri kabla serikali haijachukua hatua dhidi yao.

Baada ya muda huo, serikali italazimika kuwakamata viongozi wote waliohusika katika kuwatapeli wakulima wa zao hilo la korosho na kuwataka wenyeviti wa Amcos kumpelekea taarifa ya watendaji wa vijiji waliochukua fedha za wakulima kwa kisingizio cha kutoa huduma ya kugonga mihuri.

Alisema katika Amcos ya Mlingoti Magharibi kuna wakulima zaidi ya 30 wanalalamika kukosa sulphur wakati wameshatoa fedha zao kwa ajili ya kupata dawa hizo, lakini viongozi wa Amcos hiyo wameshinda kuwapatia wakulima hao.

Sambamba na hilo, Mkuu huyo wa wilaya amepiga marufuku Amcos zote kujihusisha kufanya biashara ya sulphur, badala yake wanatakiwa kusimamia upatikanaji wa dawa hizo ili kila mwanachama apate na kuzitumia kwenye shughuli zake za kilimo.

Chanzo: habarileo.co.tz