Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tunduru wanavyopambana na mimba shuleni

43851 Pic+tunduru Tunduru wanavyopambana na mimba shuleni

Tue, 26 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Riziki Khalifa (16) anapata uchungu akikumbuka kwamba amevuruga ndoto za kuendelea na masomo lakini pia kwa sasa analea mtoto ambaye baba yake amemtelekeza.

Alikuwa mwanafunzi wa kidato cha nne Shule ya Sekondari ya Frank Weston ya Tunduru mkoani Ruvuma ambako alifukuzwa akikaribia kabisa kufanya mitihani ya mwisho ya kidato cha nne mwaka jana.

“Natamani kama ningepata nafasi ya kuendelea na masomo ili niweze kutimiza ndoto zangu. Naumia nimepoteza ndoto zangu na kuharibu maisha yangu kutokana na kupata ujauzito nikiwa shuleni.

Sasa analea mtoto wa kiume mwenye umri wa miezi minne, Nasir, na kinachomkera zaidi ni kwamba mama yake ambaye ni mjane ndiye anayewalea wote wawili.

Akilengwalengwa na machozi, anasimulia ya kuwa vishawishi, na hasa, ujinga, ndio uliochangia kumharibia maisha.

Alipata ujauzito kwenye likizo ya Desemba 2017 wakati akijiandaa kuingia kidato cha nne. Kabla alikuwa kati ya wanafunzi waliokuwa wakifanya vizuri kwani katika mitihani ya mwisho ya kumaliza kidato cha tatu alikuwa mshindi wa saba kati ya wanafunzi 56.

Kabla ya kufukuzwa, alikuwa amefanikiwa kufanya mtihani wa majaribio bila kubainika lakini pamoja na kujitahidi kuficha ujauzito wake kwa kuvaa jubaa ambalo lilimfichia siri, mimba ilipofikisha miezi saba aligundulika na akafukuzwa.

Sasa majuto yamekuwa mjukuu, anatamani angepatikana msamaria mwema au taasisi ya kumwezesha kurudu shule akiahidi kwamba hatorudia tena mchezo wa mapenzi shuleni.

“Nimejifunza. Nipo tayari kurudi shuleni hata sasa hivi. Ukweli maisha hapa nyumbani ni magumu. Nimemuongezea mama yangu mzigo mkubwa,” anasema Riziki.

Simulizi ya Anifa Suleiman

Kwa upande wake Anifa Suleiman (15) aliyekatisha masomo akiwa kidato cha kwanza mwaka 2018 katika Shule ya Sekondari ya Frank Weston, anasema anajiandaa kujifungua watoto mapacha kama Mungu atamsaidia .

Anasema, hali duni ndiyo iliyochangia yeye kukatisha masomo kwani alijiingiza kwenye mambo ya ngono ili aweze kupata pesa ya kununua mboga na mahitaji mengine ya nyumbani kutokana na mama yake kutokuwa na kazi .

Anasema mwanaume aliyempa mimba alikuwa fundi gereji ambaye baada ya kusikia amepata ujauzito alimkimbia na kumuacha akiteseka peke yake hadi alipofukuzwa shule.

Anasema kabla ya kubainika kuwa ni mjamzito alikuwa akitoroka nyumbani na kwenda kwa wanaume akiwamo huyo fundi gereji kwa ujira wa kati ya shilingi 5,000 na 10,000.

Lakini anasema sasa maisha yamekuwa magumu zaidi na amekuwa mtu wakutegemea msaada wa majirani na mama yake mzazi ambaye anafanya vibarua vya kulima. Naye anaomba wenye moyo wa huruma kumsaidia.

Mila na desturi zatajwa kuwa chanzo

Emmakulata Kule ni mwanafunzi kidato cha nne Sule ya Sekondari Mgomba anasema tatizo la mimba za utotoni zimechangiwa na mila na desturi potofu kwani wanafunzi wengi ambao wamechezwa unyago ndio wanaopata mimba na wengi wamekuwa na tabia mbaya za umalaya na hata lugha zao si nzuri.

“ Sijui huwa wanafundishwa nini huko, kwani kiukweli kwa sisi ambao hatujapitia kwenye unyago tumekuwa tikichukizwa na vitendo vya wanafunzi wenzetu kwani tabia zao ni mbaya na wengi hawana aibu wana idadi ya wanaume wengi na hawaogopi mtu .

Anaitaka serikali kutoa elimu sahihi kwa wazazi na walezi ili wawaache watoto wao waweze kuhitimu masomo bila kuchanganya maswala ya mapenzi katika umri mdogo.

Hata hivyo, Hamida Abdalah ambaye nyakanga wa msondo Kijiji cha Nanjoka, Kata ya Nanjoka, Wilaya ya Tunduru ambaye pia ndiye aliyemcheza Anifa, anasema kuchezwa ni mila na desturi zao hivyo kama wapo wanafunzi ambao wamekatisha masomo kwa ujauzito yeye au manyakanga wenzake wasibebeshwe mzigo huo.

‘Anasema kazi yao kubwa ni kuwaelekeza watoto wawe na maadili ya kuishi vema na wanajamii , wazazi na wenzi wao watakapowapata , ikiwa ni pamoja na kuwaelekeza wajiheshimu na wasome kwa bidii.

Kaimu Mkurugenzi ambaye pia ni Ofisa Elimu Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Anderson Mwalongo, anasema mwaka 2017 kulikuwa na matukio ya mimba 21 kwa shule za msingi na 48 kwa shule za sekondari katika wilaya hiyo. Mwaka 2018 kulikuwa na mimba 14 shule za msingi na 68 shule za sekondari.



Chanzo: mwananchi.co.tz