Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tumuenzi Nyerere kwa vitendo - RC Homera

Tumuenzi Nyerere Kwa Vitendo   RC Homera Tumuenzi Nyerere kwa vitendo - RC Homera

Fri, 17 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wito umetolewa kwa jamii ya Watanzania kuenzi fikra na falsafa za Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kuwa zinaishi na kuendelea kuwa funzo kwa vizazi na vizazi.

Haya yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Kanali Dennis Mwila wakati wa Kongamano la miaka 20 ya Kumbukizi ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere iliyoandaliwa na Chuo Kikuu Mzumbe na kufanyika Jijini Mbeya.

Amesema ni dhahiri kuwa falsaza za mwalimu katika kuenzi rasilimali za Taifa na Utawala bora ni wazi kwani misingi iliyowekwa tangu Serikali ya Awamu ya Kwanza inasimamiwa mpaka sasa.

“Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ni kiongozi aliyeweka msingi wa uhuru wetu na kuimarisha nchi yetu na leo tunatambulika ulimwenguni kote kutokana na mchango wake mkubwa wa kuikomboa Tanzania na Afrika kwa ujumla wake” amesisitiza Homera.

Kwa upande wake Mzee Joseph Butiku Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere ambae pia alikuwa ni mtoa Mada Mkuu katika Kongamano hilo amesema Mwalimu Nyerere ameacha mafundisho mengi katika utawala bora na usimamizi wa rasilimali za nchi.

“Sote ni mashahidi Mwalimu Nyerere katika maisha yake amekuwa akisisitiza misingi ya uongozi wa kiadilifu, uwajibikaji na ushirikiano wa wananchi katika kufikia malengo ya maendeleo. Leo, tunahimizwa kuchukua mafundisho haya kama mwongozo katika shughuli zetu za kila siku” Amesisitiza Mzee Butiku.

Akiongea na jumuiya ya wafunzi walioshiriki katika Kongamano hilo ametoa rai kwao kutumia elimu na maarifa wanayopata katika kujenga kesho yao ili kuwa na Taifa lenye vijana wenye misingi ya uzalendo, uwajibika na kujitegemea.

Awali, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. William Mwegoha amesema Chuo hicho kinajivunia kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuzalisha wataalamu wenye maadili na maarifa katika eneo la utawala na utawala bora.

“Tunaendelea kufundisha na kutoa elimu inayojikita katika misingi ya uwajibikaji, uwazi na usimamizi thabiti wa rasilimali za umma. Tunawaanda vijana wetu kuchota hekima za Mwalimu Nyerere na kuwajengea uwezo wa kuwa viongozi wa baadae wanaozingatia maadili na maendeleo endelevu” Prof. Mwegoha amefafanua.

Katika kongamano hilo jumla ya mada ndogo sita ziliwasilishwa na wanazuoni kutoka Chuo Kikuu Mzumbe na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ikiwa ni Mtazamo wa Mwalimu Nyerere kuhusu masuala ya Ardhi, Wanawake, Madini, viwanda na kuongozwa na kaulimbiu isemayo “Mtazamo wa Mwalimu Nyerere kuhusu utawala bora na ulinzi wa rasilimali za taifa kwa maendeleo endelevu”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live