Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tumesikitishwa na Tuhuma za Mkuu wa Mkoa Geita

L2?fit=700%2C388&ssl=1 Tumesikitishwa na Tuhuma za Mkuu wa Mkoa Geita

Wed, 24 Mar 2021 Chanzo: globalpublishers.co.tz

KAMPUNI ya Global Publishers imesikitishwa na taarifa iliyotolewa jana Jumatatu Machi 23, 2021 na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel kuwa taarifa tulizozichapisha kwenye mitandao yetu ya kijamii, zikimnukuu yeye kuhusu wananchi wa Chato/Geita kubaki nyumbani na kushuhudia zoezi la kuaga mwili wa hayati Magufuli kupitia runinga, kuwa “tumejitangazia wenyewe na ni za uongo”!

Taarifa tuliyoitoa inatokana na maelezo ya Mhe. Mkuu wa Mkoa Gabriel,aliyoyatoa jana Machi 23, 2021 asubuhi, mbele ya wanahabri mkoani humo.

Video ya kwanza inaonyesha alichokizungumza RC Gabriel na tuna mnukuu:

“Machi 25, 2021, itakuwa siku maalum kwa ajili ya wananchi kutoa heshima zao. Mkoa wa Geita umepakana na mikoa jirani, wapo wananchi wa pembezoni wana kiu ya kuja kumuaga mpendwa wao.  Kwenye tukio kubwa kama hili, wapo wananchi wenye changamoto za kiafya au ukajiona ni mzima.

“Lakini kutokana na foleni kubwa ukashindwa kupata huduma, itoshe tukae majumbani kwetu tufuatilie tukio hili, kwa sababu uwanja huo utawapokea viongozi wa dini, wana familia, viongozi wa kitaifa na wana Chato na wana Geita wachache sana kwa ajili ya kuwakilisha.” Mwisho wa kunukuu.

Baadaye akaeleza tena katika video ya pili aliyofanya mahojiano na TBC jana jioni, tuna mnukuu:

“Machi 24, wananchi wa Geita walio kandokando ya barabara utakapopita mwili wa Hayati Magufuli, wajitokeze kwa wingi katika pande zote za barabara (kulia na kushoto) na kuuaga mwili wa kiongozi huyo utakapokuwa ukipita kutokea Mwanza, Sengerema mpaka Geita.

“Machi 25, wananchi walio pembezoni mwa Geita mjini na mikoa jirani ya Kagera, Kigoma na Shinyanga ni nafasi kwao wajitokeze kwa ajili ya kuaga mwili wa Hayati Dkt. Magufuli.

“Machi 26, ambayo ndiyo siku ya kumpumzisha Hayati Magufuli, itaanza ibada ya misa katika Uwanja wa Magufuli, Chato, kisha baadaye mwili utapelekwa katika eneo maalum lililopangwa kwa ajili ya maziko. Viongozi wachache watahusika kwa sababu eneo hilo ni dogo, hivyo wananchi wengine wanaweza kushuhudia tukio hilo kupitia runinga.” – Mwisho wa kunukuu.

Tulichokiripoti ni kile alichokizungumza RC Gabriel na wala hatukuwa na lengo la kupotosha au kuzua taharuki kwa jamii kama ilivyoelezwa. Aidha, taarifa hiyo haikuripotiwa na Global Publishers pekee, bali na vyombo vingine kadhaa vya habari.

Siku zote Global Publishers, tukiwa chombo cha habari kinachoheshimika na kuaminika ndani na nje ya Tanzania, hufanya kazi zake kwa kuzingatia weledi na maadili ya uandishi wa habari na tutaendelea kulisimamia hili siku zote.

Tulimpenda Magufuli akiwa hai, tutaendelea kufanya hivyo hata akiwa hayupo na huu siyo wakati wa kuanza kufarakana. PUMZIKA KWA AMANI Dkt Magufuli, MZALENDO WA KWELI WA TAIFA LETU NA AFRIKA NZIMA.

Asanteni!

Chanzo: globalpublishers.co.tz