Kufuatia tukio la kujinyonga kwa mwanafunzi wa darasa la nne Shule ya Msingi Kambarage Halmashauri ya Mji wa Kibaha Mkoani Pwani, Tatu John lililotokea Februari 19, 2023 nyumbani kwao Mtaa wa Mkoani Mjini Kibaha ambalo mazingira yake yamegubikwa na utata dada wa marehemu ameonekana kuongeza maumivu kwa familia hiyo.
Wakizungumza na Mwandishi wa habari hizi leo wakati wanashughulikia maswala ya kuchukua mwili kwenye Hospital ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani, Tumbi ndugu wa karibu na familia hiyo wamesema kuwa usiku kucha walimskia dada wa marehemu akimwita mdogo wake kwa sauti huku akipiga godoro la kitanda ambalo walikuwa wanalala yeye na marehemu mdogo wake.
"Yeye ni mkubwa kuliko marehemu ni dada yake lakini usiku kucha alikuwa anapiga kelele akigonga godoro anamwita mdogo wake hali ambayo imeendelea kutuongezea uchungu," amesema Estar Juma.
Amesema kuwa dada yake huyo ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari, Mwanalugali Mjini Kibaha mbali na kumwita marehemu usiku kucha pia alikuwa anatamka maneno ya huzuni akiuliza maswali kuwa nini kosa lake hadi mdogo wake amemuacha hali ambayo imeendelea kuwaongezea huzuni wanandugu.
Diwani wa Viti Maalumu Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Lydia Mgaya amesema kuwa ili kumrudisha mwanafunzi huyo kwenye hali ya kawaida utakayowezesha aendelee na masomo atahakikisha anamuunganisha na wataalamu wa maswala ya saikolojia ili kumpa ushauri.
"Huyu mwanafunzi inaonekana ameathirika kisaikolojia anahitaji msaada wa ushauri hivyo nitafanya kila liwezekanalo nimkutanishe na washauri wa maswala ya saikolojia," amesema.
Amesema kuwa anaamini Jeshi la Polisi litafanya uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo na kuanika ukweli.
Mwanafunzi huyo alikutwa amejinyonga ndani ya chumba cha kulala nyumbani kwao juzi huku mazingira ya tukio hilo yakielezwa kugubikwa na utata kwakuwa mwili wake ulikutwa umepiga magoti na kichwa kikiwa kimechomekwa kwenye kamba ya chandarua tofauti na ilivyozoeleka kwa matukio kama hayo ambayo watu wanaojinyonga hukutwa wananing'inia kwenye kamba.
Kamanda wa Polisi Mkoani Pwani Piusi Lutumo alisema kuwa wanaendelea na uchunguzi Ili kubaini ukweli wa tukio hilo.