Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tuhuma za ufisadi, Madiwani Tarime wamjibu Malima

40380 Pic+tarime Tuhuma za ufisadi, Madiwani Tarime wamjibu Malima

Wed, 6 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tarime. Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Tarime mkoani Mara wamejibu tuhuma zilizoelekezwa kwao na mkuu wa mkoa huo, Adam Malima aliyedai wametafuna Sh9.5 bilioni kutoka kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Acacia North Mara.

Malima alitoa tuhuma hizo mbele ya baraza hilo Februari 1 wakati akimkaribisha mkuu mpya wa wilaya ya Tarime, Charles Kabeho, ambapo alitumia fursa hiyo kumwagiza kufuatilia ubadhirifu huo.

“DC (Kabeho) fuatilia hili na kama wakishindwa kudhibitisha fedha hizi hawafai kuwa madiwani na si wa CCM, Chadema wala CUF,” alisema.

Ubadhirifu huo ulimfanya Spika wa bunge, Job Ndugai juzi bungeni kumweleza mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche kuwa ajiandae kung’oka mwaka 2020 kutokana na kushindwa kusimamia fedha hizo.

Hata hivyo, Heche akizungumza jana na Mwananchi alisema miaka mitatu mfululizo halmashauri hiyo imepata hati safi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Nalo baraza la madiwani linaloongozwa na Chadema katika kikao chao cha juzi cha dharura walisema nyaraka walizonazo zinaonyesha halmashauri hiyo imepokea Sh9.3 bilioni na si Sh9.5 bilioni kama iliyoelezwa na Malima.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Moses Yomami alisema tangu mwaka 2016 Serikali haijawahi kupeleka hata senti moja na imekuwa inajiendesha kwa mapato ya ndani ambayo hayazidi Sh4.5 bilioni kwa mwaka.

“Tunasubiri majibu ya kamati iliyoundwa na mkuu wa mkoa tuone majibu yao tulinganishe na vielelezo vyetu toka ukaguzi wa ndani na Serikali kuu tuone ni nani anayefanya kazi ndipo tutatoa tena ufafanuzi zaidi juu ya hili analodai mkuu wa mkoa,” alisema.

Naye kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Dk Peter Nyanja alisema taarifa ya matumizi yote ya fedha itapelekwa kwa mkuu wa wilaya ikiwa na vielelezo vya kupokea na matumizi yake kama mkuu wa mkoa alivyoagiza ifanyike ili kuondoa utata uliopo.

Alisema kwa kipindi kilichodaiwa kupokewa fedha ambazo zinaelezwa hazijulikani zilipo, halmashauri imepokea Sh9.3 bilioni tangu mwaka 2016.

Hata hivyo, Malima alipoulizwa kama amepokea taarifa hizo alisema bado hazijamfikia lakini aliahidi kwenda tena wiki hii kupokea taarifa hiyo.



Chanzo: mwananchi.co.tz