Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tsh. Bilioni 268 za AfDB kujenga barabara za Kusini

AGSDSHRTDHY.png Tsh. Bilioni 268 za AfDB kujenga barabara za Kusini

Fri, 26 Nov 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

TANZANIA imesaini makubaliano ya mkopo wenye masharti nafuu wenye thamani ya dola za Marekani milioni 116.34 (takribani shilingi bilioni 268.18) kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Mnivata-Newala-Masasi mkoani Mtwara yenye urefu wa kilomita 160 kwa kiwango cha lami.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba, na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Kanda ya Mashariki Dk Abdul Kamara walisaini makubaliano, Dar es Salaam.

Tutuba alisema fedha hizo zitaongeza fedha zilizotengwa kwa ajili ya miradi inayoendelea kutekelezwa na serikali kupitia ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika kutoka takribani dola za Marekani bilioni 2.27 hadi kufikia dola za Marekani bilioni 2.39.

Alisema fedha hizo pia zitatumika kujenga daraja la mto Mwiti lenye urefu wa mita 84, ujenzi wa stendi mpya za mabasi katika wilaya tatu (3) za Tandahimba, Newala na Masasi zinazonufaika na mradi, ununuzi wa magari mawili (2) ya kubebea wagonjwa, mashine mbili (2) za X-ray za kupima wagonjwa, utekelezaji wa mikakati ya usalama barabarani na mafunzo ya ujasiriamali kwa wanawake na vijana.

Alisema gharama za utekelezaji wa mradi huo ni dola za Marekani milioni 119.65 na kwamba AfDB imetoa dola za Marekani milioni 116.34 na Serikali ya Tanzania itachangia dola za Marekani milioni 3.31. Tutuba alisema utekelezaji wa mradi huo unalenga kuimarisha miundombinu ya usafirishaji katika ushoroba wa maendeleo wa Mtwara na kuchochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii na kupunguza umasikini kwa wananchi.

Alisema kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo kutaunganisha Bandari ya Mtwara na Mikoa ya Kusini mwa Tanzania na kufungua masoko ya kikanda katika nchi za Msumbiji na Malawi. Kwa mujibu wa Tutuba alisema kukamilika kwa mradi huo kutarahisisha shughuli za uchumi ikiwemo utafiti wa gesi, usafirishaji wa saruji, bidhaa za viwandani, na mazao ya kilimo likiwemo zao la korosho.

Tutuba alisema Serikali itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Benki ya Maendeleo ya Afrika ili kuimarisha ushirikiano wa kimaendeleo. Naibu Mkurugenzi Mkuu wa AfDB Kanda ya Mashariki, Dk Abdual Kamara alisema kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo kutaendeleza maeneo ya vijijini kwenye ukanda huo wa Maendeleo wa Mtwara na kufanya eneo lote la barabara ya lami kufikia kilometa 816.

Dk Kamara alisema mradi huo unatarajiwa kuleta manufaa katika uchumi wa nchi na unakadiriwa utachangia uchumi kwa zaidi ya asilimia 20.6.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live