Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tsh. Bilioni 14 zimepokelewa mkoani Tabora kukamilisha miradi

Ae2ebe7feb9b317cb48a919882f18ff2.jpeg Tsh. Bilioni 14 zimepokelewa mkoani Tabora kukamilisha miradi

Wed, 20 Oct 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Tabora, Dk Batilda Buriani amesema Serikali ya Awamu ya Sita imetoa zaidi ya shilingi bilioni 14 kwa mkoa huo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Buriani alisema hayo jana wilayani Kaliua wakati akitoa salamu za serikali kwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni mlezi wa chama wa Mkoa wa Tabora, Afadhali Twaibu Afadhali.

Afadhali alikuwa katika ziara ya ukaguzi wa utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM kwenye miradi ya maendeleo wilayani humo.

Mkuu wa mkoa alisema serikali imetoa Sh bilioni 11.7 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya madarasa katika wilaya zote.

Alisema fedha hizo zinatolewa kupitia Mpango wa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona.

Alisema Tabora ilikuwa ikikabiliwa na upungufu wa madarasa 585 na kwamba fedha hizo zitasaidia kumaliza changamoto hiyo.

Alisema Serikali ya Awamu ya Sita kila mwezi inatoa Sh milioni 900 kwa Mkoa wa Tabora kwa ajili ya elimu bila malipo ambazo zimesaidia kuongeza maudhurio ya wanafunzi.

Dk Buriani alisema serikali pia imetoa Sh bilioni moja kwa ajili ya kuanza kujenga Kituo cha Afya cha Igagala na Kashishi wilayani Kaliua.

Katika hatua nyingine, alisema wako katika mkakati wa kulima michikichi katika Wilaya ya Kaliua ili kukabili upungufu wa mafuta ya kula.

Alisema wanashirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Tumbi itakayotoa mbegu bora za michikichi kwa wakulima ambao wako tayari ili waweze kulima zao hilo.

Dk Buriani alisema pia wameanza kuhamasisha wakulima wa tumbaku walime ekari mbili za alizeti ili kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kula.

Chanzo: www.habarileo.co.tz