Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), imewekeza Sh trilioni 1.1 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya majisafi na usafi wa mazingira Dar es Salaam na Pwani pamoja na shughuli za uendeshaji na uboreshaji wa utoaji wa huduma.
Hayo yalisemwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Cyprian Luhemeja, wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Dawasa kwa mwaka wa fedha 2021/22 pamoja na kuelezea mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2022/23.
Alisema lengo la mamlaka kufanya uwekezaji huo ni kuhakikisha huduma ya majisafi kwa wakazi wa Dar es Salaam na Pwani inapatikana kwa asilimia 100 ifikapo mwaka 2023.
Alisema kwa sasa upatikanaji wa huduma ya majisafi umeimarika kwa asilimia 96 kwa Dar es Salaam na Pwani, kutokana na mpango biashara unaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu (2021/22-2023/24).
Alisema mamlaka imejiwekea malengo ya kuhakikisha huduma ya majisafi inapatikana kwa asilimia 100 pamoja na huduma ya usafi wa mazingira inaboreshwa kufikia asilimia 60 katika eneo lake la huduma.
"Tumefanikiwa kutoa huduma kwa asilimia 96, hivyo tuko mbele ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi inayoelekeza upatikanaji wa huduma ya majisafi ifikapo mwaka 2025 uwe asilimia 95 kwa mijini na asilimia 85 kwa vijijini," alisema.
Alisema mafanikio hayo yametokana na kazi kubwa iliyofanywa na mamlaka kupitia wahandisi wake wa ndani ya kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo upanuzi wa mitambo ya kuzalisha maji ya Ruvu Juu na Ruvu Chini.
Pia alitaja ujenzi wa mtandao wa mabomba wa kilometa 4,700 na ujenzi wa matangi ya kuhifadhi maji kwenye maeneo mbalimbali ya huduma.
Aidha, alisema kazi hiyo imechochea kuongezeka kwa idadi ya wateja kutoka 217,766 mwaka 2018 hadi kufikia 370,982 mwaka 2022.
Alibainisha kuwa miradi ya kimkakati iliyotekelezwa na kuanza kutoa huduma kwa wananchi ni pamoja na mradi wa kusambaza maji Makongo hadi Bagamoyo, Jeti - Buza, Mkuranga, Pugu - Gongo la Mboto, Kibamba - Kisarawe, Mlandizi - Chalinze - Mboga, Mbwawa, Soga na Zegereni.
"Kwa mwaka huu wa fedha 2022/23, Dawasa inakusudia kuanza utekelezaji wa mradi wa bwawa la Kidunda ambapo Oktoba mkandarasi ataanza kazi rasmi. Mradi huu wa kimkakati utasaidia kuongeza upatikanaji wa maji kwa Dar es Salaam na Pwani kwa asilimia kubwa na hivyo kuweka uhakika wa upatikanaji wa maji kwa kipindi chote cha mwaka," alisema.