Abiria wanaotumia usafiri wa reli ya kati kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya Kigoma na Tabora wamekwama jijini Dodoma baada ya treni ya mizigo kupata ajali mkoani Singida.
Abiria hao wapatao 1,417 wamekwama wameshindwa kuendelea na safari yao jana Oktoba 9, 2023 baada ya kupewa taarifa kuwa kuna ajali eneo la Makutupora na Saranda mkoani Singida.
Wakizungumza kwenye Stesheni ya Dodoma, baadhi ya abiria hao wamesema wanaishi katika mazingira magumu, kwani hawatarajia kukwama muda mrefu kwenye stesheni hiyo.
Abiria Shukrani Dotto anayesafiri kutoka Morogoro kwenda Kigoma, amesema walipofika Dodoma walipewa taarifa kuwa kuna ajali hivyo hawawezi kuendelea na safari mpaka saa saba mchana hivyo imewalazimu kusubiri.
Amesema mpaka leo Jumanne hawajaondoka na hawajui wataondoka saa ngapi kwa maana hakuna taarifa rasmi inayooyesha kuwa wataondoka muda gani.
Sauda Selemani anayetoka Dar es Salaam kwenda Kigoma, amesema wametumia fedha mpaka zimewaishia kwa sababu hawakutarajia kupata changamoto hiyo njiani, hivyo akiba yote waliyobeba imeshawaishia.
Amesema chakula kinachopatikana stesheni hapo kinauzwa bei ghali hata pesa wanazopewa na TRC kwa ajili ya kujikimu Sh6,000 na Sh5,000 hazitoshi kwa sababu wengine wana watoto wadogo ambao hawapewi pesa hizo.
“Kwa mfano mimi nina watoto wanne wananipa Sh5,000 kwa ajili ya kujikimu haitoshi ni bora wafanye hayo matengenezo haraka ili tuendelee na safari maana kuendelea kukaa hapa tunamaliza pesa zote,” amesema Selemani.
Abiria mwingine Rashid Kassim amesema uongozi wa TRC utoe ratiba kamili ya wao kuondoka kuliko kuwaambia wataondoka na hakuna dalili zozote za wao kuendelea na safari.
Naye, Amina Chigoji mkazi wa Chikombo jijini Dodoma amesema wanaopewa fedha ya kujikimu ni wale waliotoka Dar es Salaam na Morogoro huku wao waliokatia tiketi Dodoma wakinyimwa.
Amesema alikata tiketi ya kwenda Kazuramimba siku ya Jumapili ili asafiri jana Jumatatu lakini akakuta huo mkwamo wa safari lakini wakati wenzake wanapewa fedha za kujikimu yeye anaambiwa kuwa hakuna pesa yake.
Akijibu malalamiko ya abiria hao, Mkuu wa Stesheni ya Dodoma, Festo Mgomapayo amesema jitihada zinaendelea kuondoa mabehewa ya mizigo yaliyoanguka ili safari iendelee wakati wowote shughuli hiyo itakapopatikana.
Amewataka wasafiri hao kuvuta subira kwani taarifa walizonazo kutoka eneo la tukio zinaonyesha matumaini kuwa safari inaweza kuanza muda wowote.
Mgomapayo amesema eneo ambalo treni hiyo ya mizigo imepata ajali kuna gema na ndiyo maana suala la kuyaondoa mabehewa hayo limechukua muda kutokana na mazingira ya eneo la ajali.